Kampuni ya Saruji Mbeya (Mbeya Cement Company Limited-MCCL) imetangaza malipo ya gawio kwa wanahisa wake muongo mmoja baada ya malipo hayo kufanyika mara ya mwisho.
Kampuni hiyo imetangaza mgawo wa Sh4,259 kwa kila hisa ambayo ni faida iliyosubiriwa kwa muda mrefu inayoakisi utendaji thabiti wa kampuni uliorekodiwa mwaka wa 2023.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumamosi Juni 01, 2024 inasema malipo hayo yanaashiria mabadiliko makubwa tangu mgawo wa mwisho uliotolewa mwaka wa 2014, na ubora wa mikakati iliyofanikiwa chini ya umiliki mpya.
Kampuni hiyo inayosifika kwa chapa yake ya Tembo Cement hivi karibuni imekuwa mwanachama wa kampuni za Amsons Group ambayo ilipata asilimia 65 ya hisa kutoka kampuni za Holcim yenye makao yake makuu nchini Uswizi.
Upataji huo wa hisa ndiyo ambao umetajwa kuchochea mafanikio hayo ambayo yalienda sambamba na kuleta uongozi mpya na mikakati bunifu iliyopelekea faida za kifedha.
Taarifa hiyo inazidi kueleza kuwa mafanikio hayo yanachangiwa na kupungua kwa utegemezi wa kununua klinka (Rasilimali zinazotumika kukazia bidhaa za saruji) huku kampuni hiyo ikiongeza uzalishaji kutoka kwenye migodi yake.
“Pamoja na jumla ya mali iliyofikia Shilingi bilioni 175.2 na madeni ya Shilingi bilioni 123.8, umiliki (uwiano wa mali) wa MCCL ni wa Shilingi bilioni 51” Inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo inasema serikali ambayo inamiliki asilimia 25 ya hisa kupitia Msajili wa Hazina inatarajiwa kupata gawio la Shilingi bilioni 3, huku Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambalo lilikuwa na asilimia 10 ya hisa limepangwa kupata gawio la Shilingi bilioni 1.2.
Kukua kwake kifedha hivi karibuni kunatajwa kusaidiwa pia na makubaliano muhimu ya msamaha wa madeni, yaliyofikiwa mnamo Novemba 2023 ambayo yalibadilisha mkopo uliokuwepo kutoka kampuni ya Cemasco Limited,hivyo kurahisisha mzigo wa deni la kampuni kupungua na kuruhusu kuwekeza tena katika maeneo ya ukuaji.
Kampuni ya Mbeya Cement imedhamiria kuhakikisha ukuaji endelevu kwa miaka ijayo kwa manufaa ya wadau wake wote huku ikiongeza thamani yake kwa wanahisa, kwa kuwa na mikakati ya kujitangaza na kujiuza ili kuwabakisha wateja waliopo na kuvutia wapya