Latest Posts

MBIO ZA MWENGE WA UHURU KUFIKA HALMASHAURI SABA ZA MKOA WA ARUSHA

Ijumaa Julai 19.2024 Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amekabidhi rasmi Mwenge wa Uhuru kwa Kaimu Mkuu wa mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu kwa ajili ya kuanza kukimbizwa kwenye mkoa wa Arusha

Akizungumza wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru Kaimu Mkuu wa mkoa wa Arusha Nurdin Babu amesema ukiwa mkoani humo Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kukimbizwa kwenye Halmashauri zote saba za mkoa huo ambazo ni Halmashauri ya Meru, Halmashauri ya wilaya Arusha, Halmashauri ya wilaya Longido, Halmashauri ya jiji la Arusha, Halmashauri ya wilaya Monduli, Halmashauri ya wilaya Karatu na Halmashauri ya wilaya Ngorongoro, ambapo leo, unaanza kukimbizwa kwenye Halmashauri ya Meru

Ukiwa mkoani humo Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwa umbali wa kilomita 1,189.35, ukitarajiwa kufikia jumla miradi ya maendeleo 65, iliyogharimu shilingi za Tanzania bilioni 61.6, ambapo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu (2024) anatarajiwa kuweka mawe ya msingi miradi 18, kufungua mradi 1, kuzindua miradi 12 na kutembelea miradi 34 ya sekta za elimu, afya, maji, miundombinu ya Barabara, uwezeshaji vijana kiuchumi, Biashara na ujasiriamali, lishe, klabu za vijana wapinga rushwa, makundi maalum, uhifadhi wa mazingira sambamba na kutoa salamu na ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 katika Halmashauri zote za mkoa huo, pia Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kutembelea miradi ya maendeleo iliyowekwa mawe ya msingi na kuzinduliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka uliopita (2023).

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha imetoa mchanganuo wa miradi itakayofikiwa na Mwenge wa Uhuru 2024 kwa kueleza kuwa katika Halmashauri ya Meru utakimbizwa km 95.6 ukifikia miradi tisa (9) iliyogharimu bilioni 8.38, Halmashauri ya wilaya Arusha utakimbizwa kwa km 145.3 ukifikia miradi tisa (9) iliyogharimu bilioni 9.09, Halmashauri ya wilaya Longido utakimbizwa kwenye umbali wa km 184 ukifikia miradi nane (8) iliyogharimu bilioni 6.42 na Halmashauri ya jiji la Arusha utakimbizwa kwa umbali wa km 86.5 ukifikia miradi 10 yenye thamani ya shilingi bilioni 18.2

Kwingineko, Halmashauri ya wilaya Monduli Mwenge wa Uhuru 2024 unatarajiwa kukimbizwa kwa umbali wa km 137.3 ukifikia miradi 10 yenye thamani ya bilioni 6.08, Halmashauri ya wilaya Karatu utakimbizwa kwa umbali wa km 248.65 ukifikia miradi nane (8) yenye thamani ya shilingi bilioni 2.93 na Halmashauri ya wilaya Ngorongoro utakimbizwa umbali wa km 292 ukifikia miradi 11 yenye thamani ya shilingi bilioni 10.42

Ikumbukwe kuwa, Mwenge wa Uhuru 2024 unaadhimisha kumbukizi ya 60 tatu yaani kuadhimisha miaka 60 ya mbio za Mwenge wa Uhuru, kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar iliyozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumbukizi ya miaka 60 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, ambapo mbio zake zinahamasisha Watanzania wote kuimarisha na kudumisha umoja na mshikamano, kwa kutanguliza mbele uzalendo na kulinda tunu ya amani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kwa mwaka huu (2024) mbio za Mwenge wa Uhuru zinaenda na kauli mbiu isemayo ‘Tunza Mazingira, Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa ujenzi wa Taifa endelevu’, sambamba na hilo Mwenge wa Uhuru unaendelea kutembea na kauli mbiu za kudumu ambazo ni ‘Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Malaria, matumizi ya Dawa za Kulevya, mapambano ya VVU/UKIMWI, mapambano ya Rushwa’, sambamba na kuhamasisha wananchi kuzingatia ‘Lishe bora’, ikiwemo na kujiandaa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!