Latest Posts

MBOWE, LISSU WARUDISHWA DAR KWA ULINZI WA POLISI, BAVICHA BAADHI HAWAJAACHIWA

Na Amani Hamisi Mjege.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimethibitisha kuachiwa huru kwa viongozi wake waliokamatwa mkoani Mbeya akiwamo mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (bara), Tundu Lissu na kwamba wamerudishwa jijini Dar es Salaam kwa ulinzi wa polisi.

Taarifa ya CHADEMA iliyochapishwa siku ya Jumanne Agosti 13, 2024 katika akaunti yake ya X zamani Twitter imeeleza kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wamesafirishwa usiku kwa njia ya barabara na kupokelewa Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam ambako walitakiwa kujidhamini wakafanya hivyo kisha wakapelekwa majumbani mwao asubuhi ya Jumanne.

Hata hivyo taarifa hiyo imeeleza kuwa ofisi za CHADEMA Mbeya bado zimezingirwa na polisi ambao hawaruhusu watu kuingia katika ofisi hizo.

Wakati hilo linatokea Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema kupitia akaunti yake ya X zamani Twitter amesema kuwa kuna taarifa za baadhi ya viongozi wa Bavicha (Baraza la Vijana la Chadema) kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mbeya.

Viongozi hao ni wachache kati ya kundi la wanachama 520 waliokamatwa na polisi kwa madai ya kukiuka zuio la kutofanyika kwa kongamano la maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani inayosheherekewa Agosti 12 ya kila mwaka.

Agosti 12, 2024 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Awadh Haji alitangaza kuachiwa kwa viongozi hao na baadhi ya makada huku akionya kuwa polisi haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!