Maafisa Maendeleo ya Jamii katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wametakiwa kuwasaidia wananchi kwa kuwapa elimu ya mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri ili wananchi hao waweze kupata mkopo dirisha linapofunguliwa.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Mtwara mjini Hassan Mtenga wakati wa kukabidhi vifaa vya ujenzi wa ofisi za Serikali za Mitaa katika kata ya Mtawanya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Amesema maafisa hao wawape elimu wananchi juu ya mfumo mpya wa ukopaji pesa ambao utaanza kutumika baada ya kufunguliwa kwa dirisha la mkopo.
“Dirisha la mikopo lilifungwa kwa muda kwa ajili ya kurekebisha kutokana na Rais kugundua kuwa mikopo ina ujanja mwingi,watu wanaomba karibia miaka 10 lakini wanasema sifa hawana lakini ni wafanyabiashara,sasa maafisa maendeleo kuweni walimu muwafundishe hawa huu mfumo mpya” Amesema Mtenga.
Afisa Maendeleo kata ya Mtawanya kwenye manispaa hiyo, Frolah Mwanicheta amesema lengo kubwa la mkopo huo ni kuwainua kiuchumi wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambao watakuwa kwenye kikundi ambacho kimesajiliwa, na tayari wanashughulikia uzalishaji ambao utawawezesha kulipa mkopo.
Sambamba na hilo wananchi wa kata hiyo wamemuomba Mbunge huyo kuwatatulia changamoto ya maji ambayo imekuwa kilio chao cha muda mrefu licha ya kuwa chanzo cha maji kipo kwenye kata hiyo.
Akijibu kwa njia ya simu baada ya kupigiwa na mbunge huyo kuhusu changamoto hiyo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA) Mhandisi Rejea Ngo’ndya amesema Julai 18, 2024 atafika kwenye maeneo yote ambayo maji hayafiki kwenye kata hiyo kwa ajili ya kujua tatizo.
Vifaa hivyo vya ujenzi wa ofisi za Serikali za Mitaa vilivyotolewa ni mabati 160 ambapo kila mtaa bati 40, mifuko ya saruji 15 na tofali 500 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya shule ya msingi Majengo iliyopo kata ya Tandika kwenye manispaa hiyo. Hata hivyo kata ya Mtawanya ametoa mabati 150, saruji mifuko 45 na tofali 1500 kwa mitaa minne