Mbunge wa jimbo la Msalala Iddi Kassim Iddi ameutaka mgodi wa kijiji cha Ndala, uliopo kata ya Shilela pamoja na SHIREMA (Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Dhahabu mkoa wa Shinyanga) kutekeleza takwa la kisheria la kutoa asilimia 10 ya mapato ya mgodi huo kwa kijiji cha Ndala.
Hatua hiyo inakuja baada ya taarifa ya Mtendaji wa kijiji cha Ndala kuonesha kuwa tangu uchimbaji wa madini umeanza kijijini hapo mpaka sasa fedha ambazo zimelipwa na mgodi huo ni takribani shilingi milioni nne pekee.
Mbunge Iddi ameonesha kuingiwa na mashaka juu ya mfumo wa ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya asilimia 10 ya mgodi huo kwa ajili ya kijiji cha Ndala wakati akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, ambapo alibaini hayo baada ya kusikiliza kero zao
“Niwaombe wananchi wa kata ya Shilela undeni vikundi ambavyo vitaweza kusimamia pindi zinapotokea ‘rashi’ kwenye maeneo haya SHIREMA ni sawa na kikundi, leo mngekuwa na kikundi mngeweza kusimamia wenyewe mapato ambayo yanapatikana kwenye mgodi uchimbaji unafanyika akaunti ya kijiji inakuwa na milioni 4 tu kweli jamani hata kama wewe ungekuwa ndio msimamizi niwahakikishie hapa lazima pesa zitarudi tu” Amesema mbunge Iddi.
Aidha, Mbunge huyo amesema kuna baadhi ya viongozi wa kata hiyo pia walikuwa na mgao kwenye mgodi wa kijiji suala ambalo yawezekana kukawa na upigaji ambao unapelekea kudhorotesha maendeleo ya kijiji pamoja na kuwepo kwa rasrimali madini ambazo ni chanzo kikubwa cha mapato ndani ya kijiji.
Mbunge Iddi amesema kama tatizo lipo kwenye SHIREMA yeye binafsi atahakikisha anafuatilia kwa viongozi ambao wamepewa majukumu ya kusimamia mgodi kwa lengo la kujua asilimia 10 za kijiji zinapatikana kwa wakati na zinafanya kazi za maendeleo ambayo yamekusudiwa kwenye Kijiji hicho.