Mbunge wa Dadaab nchini Kenya, Farah Maalim amefukuzwa kutoka hoteli ya Sarovah Whitesands Beach Resort mjini Mombasa alikokuwa akiishi kutokana na matamshi ya kutatanisha aliyoyatoa hivi karibuni dhidi ya vijana wa Kenya wanaoandamana.
Kulingana na vyombo vya habari vya Kenya, matamshi hayo aliyatoa kwenye video inayosambaa kwa kasi mtandaoni ambayo imezua hasira kwa vijana na wananchi wa Kenya kwa ujumla, hata hivyo bado haijajulikana ni lini haswa video hiyo ilirekodiwa.
Ripoti zinaonesha kuwa mbunge huyo aliingia hotelini siku ya Ijumaa. Mkurugenzi Mkuu wa Sarovah Hotels Jimi Kariuki alitoa tangazo la kufukuzwa kwa mbunge huyo katika mtandao wa X zamani Twitter baada ya baadhi ya watumiaji wake kuishutumu hoteli hiyo kwa kumruhusu kukaa hapo.
Kariuki alisema kwa uwazi kuwa hoteli haiungi mkono kwa vyovyote vile matamshi tata ya Maalim.
“Habari za jioni. Yeye si mgeni tena katika hoteli yetu. Tulimwomba aondoke hotelini mapema mchana. Kwa vyovyote vile hatuungi mkono kauli zake za uchochezi na vitisho dhidi ya Wakenya na hatutahusisha chapa yetu na mtu kama huyo” Aliandika Kariuki.
Katika video hiyo Maalim alionekana akizungumza kwa lahaja ya Kisomali kuwa kama angekuwa Rais wa Kenya angechinja waandamanaji 5,000 kila siku.
Tafsiri ya lugha ya video hiyo iliyothibitishwa ilifichua kuwa mbunge huyo alikuwa akiwashutumu vijana wa Kenya ‘Gen Z) kwa jaribio lao la kuandamana hadi Ikulu wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa fedha wa 2024.
“Hili lilikuwa jaribio la mapinduzi, jaribio la wazi la mapinduzi. Watoto wa wamiliki matajiri wa biashara, wazazi matajiri na watoto waliolelewa kwa mali iliyopatikana kwa njia isiyo sahihi, 80% kutoka kabila moja waliachwa katikati mwa jiji na kuambiwa wafanye ghasia na kushikilia majengo ya Ikulu na Bunge, Mungu apishe mbali, ningekuwa rais ningewachinja, 5,000 kila siku” Alisema.
Maalim amejitetea akisema video hiyo ilihaririwa ili kumchora kwa picha mbaya.
“Yote ni kuhariri, kukata na kupesti, kuchukua neno kutoka hapa, jingine kutoka hapa na kuweka pamoja. Kuna upuuzi mwingi sana. Kimsingi ni Wasomali ambao wangefanya hivyo kwa sababu niliingilia siasa zao. Siyo picha ya kweli,” Alijitetea Maalim.
Kufuatia tuhuma hizo, Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ilimuita ili kuangazia maoni yake yenye utata huku Kamati Kuu ya Kitaifa ya chama cha Wiper (NEC) ikitaka Maalim afurushwe kutoka kwa wanachama wa vyama vya upinzani kutokana na matamshi hayo.