Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Esther Malleko, ametimiza ahadi yake kwa wanawake wa mkoa huo kwa kuwakabidhi jumla ya mashine 169 za kutotolesha vifaranga vya kuku (incubators), zenye thamani ya shilingi milioni 84.5 kwa kata zote 169 za Mkoa wa Kilimanjaro.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Aprili 13, 2025, Malleko pia ameahidi kuwapatia wanawake hao mitaji ya mayai ya kuanzia mradi huo na watalamu wa kuwapa mafunzo ya matumizi sahihi ya mashine hizo, ufugaji bora wa kuku na utunzaji wa fedha ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija na kubadilisha maisha ya wanawake wa Kilimanjaro.
“Wanawake wa Kilimanjaro mlinikopesha imani, leo nimekuja kuilipa kwa vitendo. Hizi incubator 169 zenye thamani ya milioni 84.5 ni zetu, ni za maendeleo yenu, ni sehemu ya ahadi yangu kwenu ili muweze kuondokana na mikopo ya kausha damu na kuwa huru kiuchumi, kiafya na kijamii,” amesema Malleko.
Malleko pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa alioufanya mkoani Kilimanjaro, akitaja miradi ya maji Same-Mwanga-Kilimanjaro, ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, madarasa, miundombinu ya barabara na sekta ya utalii.
“Wanawake wa Kilimanjaro hatuna deni na Rais Samia. Tunaahidi kumpigia kura nyingi apate ushindi wa kishindo 2025,” amesema kwa kujiamini.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel, amempongeza Malleko kwa kutekeleza ahadi hiyo na kuwataka wanawake hao kuzitumia incubator hizo kwa uangalifu na kujiimarisha kiuchumi, huku wakiwa na hamasa ya kutafuta kura za ushindi kwa CCM.
Baadhi ya wanawake waliokabidhiwa mashine hizo wameeleza furaha yao, wakisema sasa wana uhakika wa kuboresha uchumi wa familia, kujenga afya ya jamii na kuimarisha mshikamano wa wanawake wa mkoa huo.