Mgogoro wa shamba uliodumu kwa miaka 26 kati ya mwekezaji Elizabeth Stegmaier na chama cha msingi cha ushirika Uduru Makoa lenye ukubwa wa hekari 358 unatarajiwa kumalizika mara baada ya hatua za kisheria kukamilika.
Akizungumza na Wananchi Juni 2,2025 Mbunge wa jimbo la Hai Saashisha Mafuwe amewataka wananchi wa kata ya Machame Kaskazini wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kuwa wavumilivu katika kupata haki yao ya kukabidhiwa shamba la Makoa linalomilikiwa na chama cha ushirika Uduru Makoa kutoka kwa mwekezaji Elizabeth Stegmaier ambaye anadaiwa kukiuka mkataba wa shamba hilo na kulitumia kwa manufaa yake binafsi kwa miaka ishirini na sita hivyo baada ya Mahamakama Kuu kuthibitisha kwamba shamba hilo ni la wananchi.
Saashisha amewasihi wananchi hao kutofanya vurugu yoyote na kuwa watulivu kwani kukosea hatua moja kutampa nafasi mwekezaji huyo kuendelea kuwasumbua hivyo ni vyema kuendelea kuheshimu muhimili wa Mahakama na kwamba jambo likiwa Mahakamani zipo taratibu zakufuata.
“Cha kwanza hili ni shamba letu, ni haki yetu hilo halina mjadala lakini pia Mahakama Kuu imetuthibitishia kwenye hukumu yake kuwa shamba hili ni la kwetu,lakini lenye mjadala ni hatua za makabidhiano,hatua hizi za makabidhiano tukikosea hatua moja tunampa nafasi ya yeye kuendelea kutusumbua, tunaheshimu muhimili wa mahakama,jambo likiwa mahakamani kuna namna yake kuna taratibu zake,hivyo kuweni watulivu”alisema Saashisha.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Hai Hassan Bomboko amesema mgogoro huo umepitia hatua tofauti tofauti lakini siku za hivi karibuni Mahakama Kuu imetoa maamuzi yanayoonyesha hakuna mkataba na mwekezaji huyo na kwamba shamba hilo linatakiwa kurudi katika chama cha msingi cha Ushirika cha Uduru.
Bomboko ameeleza kuwa tayari chama hicho cha msingi cha ushirika Uduru kimempatia taarifa mwekezaji huyo ya kumtaka aondoke katika eneo hilo.
“Ndugu zangu mgogoro huu umepitia hatua tofauti tofauti lakini siku za hivi karibuni mahakama kuu imetoa maamuzi ambayo inaonyesha kabisa hakuna mkataba kwa sasa na eneo hili lirudi kwa ushirika”amesema Bomboko.
Nao wananchi waliojitokeza kwaajili ya kutaka kukabidhiwa shamba hilo wamemshukuru Mbunge wa jimbo la Hai kwa namna alivyopambana kurejesha shamba hilo kwa wananchi na namna anavyotaka taratibu za kuendesha vyama vya msingi vya ushirika kufuatwa ili Wananchi wafaidi ushirika wao.