Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo amesema kutokana na jitihada nyingi zilizofanywa na serikali pamoja na taasisi mbalimbali kumsaidia mtoto wa kike kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, sasa wameanza kuweka nguvu kwa mtoto wa kiume ili kuleta usawa.
Ametoa kauli hiyo baada ya ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi inayotekelelezwa katika Shule mbalimbali Mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro ambapo ametembelea shule ya Lucy Lameck, JK Nyerere, Mwenge, Mawenzi na Msandaka.
“Tofauti na jamii ilivyozoea katika shule ya sekondari Msandaka, serikali inatarajia kujenga bweni litakalobeba wanafunzi wa kiume karibu 80 huku Manispaa ya Moshi ikiendelea kuongeza mabweni hayo kwa kadiri fedha zitakavyopatikana, tunataka kuwepo na usawa na sasa ni zamu ya Wanafunzi wa kiume” Amesema Tarimo
Amesema hivi sasa uhitaji wa kumsaidia mtoto wa kiume ni mkubwa kwani kwenye jamii mtoto wa kiume amesahaulika na ndiyo maana kasi ya ukatili kwa mtoto wa kiume imeongezeka.
Pia amesema kipitia Bunge Marathon wamekubaliana fedha zote zilizokusanywa zijenge mabweni ya wavulana ili juhudi za kumlinda mtoto wa kike ziende sambamba na mtoto wa kiume.