Latest Posts

MBWANA: WAGENI WANAENDESHA BIASHARA KINYEMELA K’KOO, WATANZANIA WANAACHWA NA MADENI

Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara na Huduma Tanzania (UWAHUTA), Martin Mbwana, amesema tatizo la raia wa kigeni kufanya biashara za machinga kinyemela katika Soko la Kariakoo limekuwa mzigo mkubwa kwa wafanyabiashara wa Kitanzania, kwani wengi wao hujikuta wakibebeshwa madeni makubwa ya kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) bila kujua.

Akizungumza katika mahojiano na Crown FM, Mbwana amesema wageni hao huendesha biashara kwa kutumia majina ya wenyeji wa Kitanzania, lakini baadaye huondoka nchini na kuwaacha wafanyabiashara wazawa wakikumbwa na mzigo wa kodi.

“Tulikuwa tunasema, wewe uko mbele ya duka, kila kitu kinasoma jina lako. Lakini yule mgeni anakufuata nyuma taratibu, anafanya biashara, mwishoni anachukua briefcase yake na kuondoka. Wakati huo TRA inakukadiria deni la Shilingi milioni 200, 300 au hata 500. Hili ni tatizo kubwa,” amesema Mbwana.

Mbwana amesisitiza kuwa njia pekee ya kukabiliana na changamoto hiyo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanasajili biashara zao rasmi kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili kujilinda kisheria.

“Tunawashauri wafanyabiashara wasajili biashara zao BRELA kwa kufuata taratibu zote za kisheria. Hii itawapa uhalali wa biashara na kuwaepusha na matatizo ya madeni yasiyo yao. Kama unashirikiana na mgeni, hakikisha kila kitu kiko wazi kisheria na BRELA iwe na taarifa,” ameongeza.

Amebainisha kuwa elimu kwa wafanyabiashara juu ya usajili wa biashara ni muhimu ili kuwalinda na kuhakikisha wanakuwa sehemu ya mfumo rasmi wa biashara nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!