Latest Posts

MCHENGERWA AAHIDI MAGEUZI AKIWASILISHA BAJETI YA TAMISEMI TRILIONI 11.78

Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26 yenye jumla ya shilingi trilioni 11.783, ikiwa ni ongezeko kutoka trilioni 10.125 za mwaka wa fedha uliopita. Bajeti hiyo imepanda kwa zaidi ya trilioni 1.66.

Akiwasilisha bajeti hiyo Aprili 16, 2025 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, amesema kati ya fedha hizo, trilioni 3.95 zimeombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo trilioni 2.5 ni fedha za ndani — ikijumuisha bilioni 613.44 za mapato ya ndani ya halmashauri — na trilioni 1.45 ni fedha za nje.

Kwa upande mwingine, trilioni 7.84 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, ambapo trilioni 6.3 ni kwa ajili ya mishahara na trilioni 1.53 kwa matumizi mengineyo, ikiwa ni pamoja na trilioni 1.067 za mapato ya ndani ya halmashauri.

“Tumewasilisha si tu makadirio ya mapato na matumizi, bali tumeweka mbele yetu dira ya matumaini, ramani ya maendeleo na ahadi ya uongozi unaowajibika,” amesema Mchengerwa.

Ameongeza kuwa bajeti hiyo si kwa ajili ya kutafuta sifa za kisiasa bali suluhisho kwa maisha ya Mtanzania wa kawaida. Aidha, Mchengerwa ametoa wito kwa mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wananchi wote kushirikiana kwa mshikamano katika utekelezaji wa bajeti hiyo.

“Kwa dhamira hii na kwa imani kubwa kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunawasilisha bajeti hii kama zana ya kazi, dira ya matumaini na silaha ya mapinduzi ya kiutawala, kiuchumi na kijamii,” amesisitiza.

Waziri huyo amehitimisha kwa kusisitiza kuwa TAMISEMI ndiyo msingi wa maendeleo endelevu na kila shilingi ina jukumu lake, kila kiongozi ana wajibu wake, na kila mwananchi ana nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!