Latest Posts

MCHENGERWA: WAGOMBEA WASIORIDHIKA WAWASILISHE PINGAMIZI, SI MALALAMIKO MITANDAONI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, amewataka wagombea wote ambao hawajaridhishwa na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuweka pingamizi ndani ya siku mbili kuanzia tarehe 8 hadi 9 Novemba, 2024.

Akiongea na vyombo vya habari jijini Dodoma tarehe 8 Novemba, 2024, kuhusu uteuzi wa wagombea, Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa siku ya tarehe 8 ni muhimu kwa uteuzi wa wagombea kwa mujibu wa Kanuni ya 18 ya Tangazo la Serikali Na. 571, 573, 574 pamoja na Kanuni ya 17 ya Tangazo la Serikali Na. 572, yote ya tarehe 12 Julai, 2024.

Amebainisha kuwa kanuni hizi zinamtaka Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kufanya uteuzi wa wagombea kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni. Mara baada ya uteuzi kukamilika, majina ya wagombea wenye sifa na wale wasiokidhi vigezo yatabandikwa hadharani ili umma, wakiwemo wagombea wenyewe, waweze kuyapata.

Waziri Mchengerwa amesema kuwa kwa mujibu wa kanuni, mgombea yeyote ambaye hakuridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi anaweza kuwasilisha pingamizi kwa maandishi ndani ya siku mbili tangu uamuzi ulipofanyika. Msimamizi huyo atashughulikia pingamizi hilo na kutoa uamuzi ndani ya siku mbili tangu alipolipokea.

“Hivyo, kwa mujibu wa kanuni hizi, kuanzia leo tarehe 8 na kesho tarehe 9 Novemba, 2024, kwa mgombea yeyote ambaye hatoridhika na uamuzi wa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuhusu uteuzi, anapaswa kutumia nafasi ya siku hizi mbili ili malalamiko yake yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa kanuni,” amesisitiza Waziri Mchengerwa.

Ameongeza kuwa wagombea wasioridhika wanapaswa kufuata taratibu za kisheria kwa kuweka pingamizi badala ya kupeleka malalamiko mitandaoni, kwani malalamiko yasiyofuata taratibu hayatashughulikiwa. Amewataka wagombea kuhakikisha malalamiko yao yanawasilishwa kwenye sehemu sahihi na ndani ya muda uliowekwa ili kuimarisha utulivu na uwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa Mchengerwa, iwapo mgombea hatoridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kuhusu pingamizi lake, ana haki ya kukata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ndani ya muda usiozidi siku nne baada ya uamuzi huo kutolewa. Rufaa hizo zitaanza kupokelewa kuanzia tarehe 10 hadi 13 Novemba, 2024.

Waziri Mchengerwa amehitimisha kwa kuwasisitiza wagombea wote kufuata taratibu za kisheria ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi na utulivu, hivyo kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima ambayo yanaweza kuleta changamoto katika mchakato wa uchaguzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!