Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Tanzania Bara Isihaka Mchinjita ametoa wito kwa Waziri wa Kilimo nchini Hussein Bashe kuwatafutia ASA (Wakala wa Taifa wa Mbegu) eneo maalum la kulima mbegu zake ili kuwaachia wananchi mashamba yao, hatua hiyo itawezesha wakulima kuzalisha mazao yanayotumika kulisha Watanzania
Mchinjita ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma akiendelea na ziara yake ya kutembelea mikoa sita (6) iliyoanza Julai 22.2024 ambapo ziara hiyo ina lengo la kusajili wanachama milioni 10 kwa miezi 10 na kusikiliza kero za wananchi.
“Waziri Bashe (Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo) ameanzisha mashamba ya BBT (Building a Better Tomorrow) kule Dodoma, ni vyema akaelekeza wakulima wa mbegu huko badala ya kuwafukuza wananchi na wakulima kutoka kwenye mashamba yao, kama serikali ina ardhi ya kutosha kiasi cha kuwahimiza vijana wote waliokosa ajira kuenda kulima, kwa nini wakulima wanatolewa kwenye mashamba yao?” -Mchinjita
Aidha, Mchinjita ameongeza kuwa mkoa wa Ruvuma unaongoza kwa uzalishaji wa Makaa ya mawe ambayo yanapelekwa kwenye mikoa mingine yenye viwanda, lakini mkoa huo hauna viwanda ambavyo vingesaidia kuzalisha malighafi zinazopatikana hapo, hatua ambayo ingewasaidia wananchi kupata vipato na vijana kupata ajira
Mchinjita pia amezungumzia kuhusu mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 600 kwa kutumia Makaa ya mawe, ambao haujaendelea, amesema mradi huo ungeweza kuchochea uwekezaji kwa kuhakikisha upatikanaji wa nishati na hivyo kuvutia wawekezaji kutoka Duniani kote kuwekeza katika malighafi zinazopatikana Ruvuma.