Latest Posts

MEJA JENERALI MABELE AWATAKA VIJANA WA JKT KUWA WAZALENDO NA KULINDA NCHI YAO

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, amewataka vijana wa Jeshi hilo kuwa tayari kuilinda nchi yao na kujitolea maisha yao pale taifa litakapowahitaji, akisisitiza kuwa sasa ni sehemu ya jeshi la akiba la taifa.

 

Meja Jenerali Mabele alitoa wito huo alipokuwa akifunga mafunzo ya vijana wa Mujibu wa Sheria, Operesheni Miaka 60 ya Muungano, katika Kikosi cha Msange JKT kilichopo mkoani Tabora.

Katika hotuba yake, Meja Jenerali Mabele alieleza umuhimu wa mafunzo ya JKT kwa vijana kutoka makabila na dini mbalimbali nchini. Alibainisha kuwa JKT inawajenga vijana kuwa wamoja, waaminifu kwa taifa, na wenye nidhamu, huku akisisitiza kuwa mafunzo ya JKT ni daraja la kuimarisha umoja wa kitaifa. “Tunawafundisha vijana Utanzania, hivyo nidhamu ya kuilinda nchi yetu iwe silaha kubwa mtakapoenda sehemu yoyote,” alisema Meja Jenerali Mabele.

Aidha, Kaimu Kamanda wa Brigedi ya Faru, Brigedia Jenerali Gabriel Kwiligwa, aliwaasa wahitimu kutumia mafunzo waliyopata ili kuwa mfano bora kwa jamii, na kusisitiza umuhimu wa kujiepusha na vitendo vyenye madhara kwa afya ya mwili na akili. Aliongeza, “Mkawe mfano wa kuigwa mtakaporudi nyumbani au vyuoni.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa JKT, Kanali Amos Mollo, alisema kuwa mafunzo hayo yalianza rasmi mnamo tarehe 19 Juni 2024 na kufungwa tarehe 4 Septemba 2024. Aliwashukuru wazazi kwa kuwaunga mkono vijana wao kujiunga na mafunzo ya JKT, akieleza kuwa mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kujenga uzalendo na moyo wa kulitumikia taifa.

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kanali Makame Daima, alitoa pongezi kwa mwaliko wa kushiriki hafla hiyo, akiisifu JKT kwa ushirikiano wao wa karibu. Alibainisha kuwa taasisi za JKT na JKU ni kama mapacha, kutokana na mafunzo yao yanayofanana, na akatoa mchango wa shilingi milioni tano kwa Kikosi cha Msange JKT kusaidia maendeleo ya miundombinu ya kikosi hicho. “Tunapaswa kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na vijana wetu wawe mstari wa mbele katika kuulinda na kuudumisha Muungano huu,” alisema Kanali Daima.

Naye Kamanda wa Kikosi cha Msange JKT, Kanali Sadick Mihayo, alieleza kuwa mafunzo hayo ya miezi mitatu yamewaandaa vijana kuwa na moyo wa uzalendo na nidhamu ya hali ya juu. “Vijana hawa wamefundishwa maadili ya kujenga taifa, na wameonyesha nidhamu ya hali ya juu kwa muda wote wa mafunzo,” alisema Kanali Mihayo.

Service Girl Loyce Lutamingwa, akitoa risala kwa niaba ya wenzake, aliwasihi wazazi kuona umuhimu wa mafunzo ya JKT na kusisitiza kuwa yana nafasi kubwa ya kuwajenga vijana kuwa wazalendo na tayari kulitumikia taifa. “Tumejifunza mengi, na tunaamini kuwa mafunzo haya yatatufanya tuwe raia wema na wazalendo. Ni muhimu mafunzo haya yadumishwe kwa maslahi ya vizazi vijavyo,” alisema Lutamingwa.

Katika hafla hiyo ya kufunga mafunzo, wahitimu walionesha ujuzi waliofundishwa kwa vitendo, ikiwemo gwaride na maonesho mbalimbali ya kijeshi, ikiwa ni ishara ya utayari wao katika kulitumikia taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!