Latest Posts

MELI KUBWA YAWASILI BANDARI YA MTWARA KWA AJILI YA KUSAFIRISHA MAKASHA YA KOROSHO

Meli kubwa zaidi kuwahi kufika katika Bandari ya Mtwara, yenye urefu wa mita 240, imewasili Septemba 20, 2024, ikiwa na makasha matupu zaidi ya 400 kwa ajili ya msimu wa korosho wa mwaka 2024/2025.
 
Meli hiyo imekuja kushusha makasha hayo mapema kama maandalizi ya usafirishaji wa korosho, hatua inayolenga kuhakikisha msimu wa korosho unaanza kwa ufanisi mkubwa.
 
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Mkoa wa Mtwara, Ferdinand Nyathi, amesema kuwasili mapema kwa makasha hayo ni hatua muhimu kwa wafanyabiashara wa korosho.
 
Nyathi alisema kuwa “Kuwasili kwa makasha haya mapema kutawezesha wafanyabiashara kupata makasha kwa urahisi pale ambapo minada ya korosho kwa msimu wa 2024/2025 itakapoanza.”
 
Ameongeza kuwa mwaka huu kumekuwa na mabadiliko makubwa na muitikio mkubwa kutoka kwa mawakala wa meli ambao wameleta meli zao mapema, tofauti na mwaka jana ambapo meli zilianza kufika mwishoni mwa Oktoba.
 
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amezungumza pia kuhusu umuhimu wa kuwasili kwa makasha hayo, akibainisha kuwa ni ishara kwamba wasafirishaji wako tayari kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha korosho inasafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara.
Telack amewahakikishia wanunuzi wa korosho kuwa vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya usafirishaji wa korosho vitakuwepo kwa wakati, na kwamba changamoto zote zilizojitokeza msimu uliopita zimeshafanyiwa kazi.
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Rajabu Kundya, ameongeza kuwa kuwasili kwa meli kubwa katika Bandari ya Mtwara ni kiashiria cha kukua kwa bandari hiyo.
 
“Kuwasili kwa meli hii kubwa zaidi yenye urefu wa mita 240 ni kiashiria cha maendeleo makubwa katika Bandari ya Mtwara, na ni mara ya kwanza kwa bandari hii kupokea meli ya ukubwa huu tangu ilipoanza kufanya kazi,” amesema Kundya.
 
Kuwasili kwa meli hiyo kunatarajiwa kusaidia kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa zao la korosho nje ya nchi kwa ufanisi zaidi msimu huu wa mwaka 2024/2025.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!