Latest Posts

MEYA AAGIZA UCHUNGUZI MILIONI 35 ZILIZOINGIZWA AKAUNTI YA WAZAZI

Baraza la Madiwani Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara kupitia Meya wa Manispaa hiyo Shadida Ndile limeomba vyombo vya usalama kuchunguza matumizi ya fedha Shilingi milioni 35 zilizoombwa na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini Hassan Mtenga kwa ajili ya ukarabati wa shule ya sekondari Shangani.

Maamuzi hayo yamefikiwa mara baada ya Diwani wa kata ya Shangani Abuu Mohamed kuomba ufafanuzi ndani ya kikao cha baraza kuhusu fedha hizo zilizoombwa kupitia shule hiyo ambazo hazijatumika kwa kufuata taratibu ikiwamo Halmashauri kutokuwa na taarifa yoyote.

“Shule ya sekondari Shangani imepokea fedha Shilingi milioni 35 kutoka Mamlaka ya Usimamizi Wa Bandari Tanzania (TPA), utaratibu unafahamika fedha za umma zinavyoingia kwenye akaunti za shule au umma vikao vitakaa, kama fedha ya vifaa watashindanishwa wazabuni, na kisha utaratibu wa manunuzi utaanza na baadaye utaratibu wa malipo utafanyika” Amesema Abuu na kuongeza,

“Lakini kwa shule ya Shangani sekondari fedha zimeingia na kwenda kwa wazabuni moja kwa moja bila kufuata utaratibu wowote, kwa maelekezo ya Mbunge kwamba hizo fedha ni zake na fedha hizi hazijaonekana sehemu yoyote kwenye taarifa zetu za halmashauri, fedha zilizotumika ni milioni 3 ya vifaa fedha nyingi imepelekwa wapi na utaratibu upi ulitumika?” Amehoji Abuu

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mwalimu Hassan Nyange amesema akaunti iliyotumika kuingiza fedha hizo ni akaunti ya wazazi na siyo ya Halmashauri na amesema kwenye taarifa ya mkuu wa shule hiyo inaonesha milioni 15 imetumika kupeleka vitu kwenye maeneo 30 na milioni 20 amepeleka vifaa mbalimbali kwenye maeneo 22 ambapo pia kuna ushahidi wa barua ya watu kukiri kupokea vifaa kwenye maeneo hayo.

Hata hivyo Meya wa Manispaa hiyo aliagiza baraza kuwa kamati ijadili taarifa hiyo kwa kina ambapo mara baada ya majadiliano walikubaliana kwa kukabidhi vyombo husika ili kufuatilia hoja hiyo.

Mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini Hassan Mtenga akijibu hoja hiyo kwa njia ya simu amesema fedha hizo hazikupitia kwenye akaunti ya Halmashauri hivyo hazipaswi kujadiliwa na madiwani kwakuwa fedha ni za Mbunge.

“Mimi ni mbunge na akaunti ninazotumia situmii akaunti ya serikali kuombea hela na wala hazipaswi wao kujadili, mimi ninakaa na wazazi na mimi naomba hela, hela ile ni ya wadau wangu siyo serikali sasa hela zangu nitafute tenda”Amesema Mtenga.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!