Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Patrobas Katambi ametoa wito kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mfumo mpya wa ununuzi wa umma wa kielektroniki (NeST) ili kuondoa urasimu na kukuza uwazi.
Katambi ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma kwenye semina ya Wabunge iliyoandaliwa na Mamlaka ya udhibiti wa ununuzi wa umma (PPRA) ambapo amesema mfumo huo ni tiba na imara kwani itasaidia kuleta maendeleo kiuchumi na kupiga vita ufisadi.
Katambi amesema mfumo huo utafanya utendaji kazi kuongezeka kwa kiasi kikubwa, usawa na ushidani kuongezeka zaidi bila kusahau uwazi katika kazi.
Ameendelea kufafanua kuwa mfumo huo utasaidia ufutiliaji ambapo mfumo wa ‘kuripoti’ hautakuwa mgumu tena kama jinsi ambavyo awali ingelazimika kwenda kuchambua makaratasi ya hapa na pale na hata data kwa jamii, wataalamu na Wabunge ambapo watakuwa na uwezo wa kupata kwa wepesi zaidi kwani data hizo sasa zitakuwa kwenye mfumo.
“Kutakuwepo kwa uzingatiwaji wa viwango hasa kwenye maeneo ya kanuni kama hazijazingatiwa mfumo utakuonyesha kama una haki ya kukata rufaa, mfumo utasaidia kuongeza viwango vya kimataifa vinavyotaka mifumo ya manunuzi kufuatwa na kuzingatiwa kwa kiwango kwani kila kitu kitafanyika kwenye mifumo ambapo uwazi wa kiasi cha juu utaonekana” Amesema Katambi.
Amesema mfumo huo utaboresha mahusiano bora ya wasambazaji au wadau wenyewe kwenye mfumo nzima kwa kuwa na mahusiano bora kwani mambo yataonekana kwenye mfumo na itaondoa urasimu
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa PPRA Eliakimu Maswi amesema mfumo huo wa NeST utaanza kutumika rasmi June 17 mwaka huu huku kanuni zake zikitarajiwa kuanza kutumika July mosi mwaka huu.