Latest Posts

MGOGORO WA KISIASA WATOKOTA KATI YA CUF NA ACT, ADO ASEMA HATAOMBA RADHI KWA KAULI ZAKE

Katika hatua ya hivi karibuni, hali ya taharuki imeibuka kati ya Chama Cha Wananchi (CUF) na ACT-Wazalendo kufuatia kauli za Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu ambazo zilidaiwa na CUF kuwa za matusi na kejeli dhidi ya CUF.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF Mohamed Ngulangwa Septemba 17, 2024 ilieleza kuwa kauli za Ado zimeibua taharuki na huzuni ndani ya chama hicho na kwamba hazikubaliki, hivyo kumtaka Ado aombe radhi hadharani.

Hata hivyo, Ado Shaibu amesisitiza kuwa hataomba radhi, akiongeza kuwa kazi ya siasa ni ya ushawishi kupitia hoja, si matusi wala vitisho, huku akilaani tamko la CUF.

“Kazi ya siasa ni kazi ya ushawishi. Ushawishi unafanywa kwa hoja sio matusi wala vitisho. Tamko la CUF lililotolewa na Mkurugenzi wake wa Habari ni ishara ya wazi ya taasisi inayokata roho. Hakuna taasisi makini ingeruhusu tamko lililosheheni matusi kama lile litoke kwa umma”, ameeleza Ado.

CUF kupitia tamko lake walisema kauli za Ado ni muendelezo wa chokochoko ambazo zimetajwa kuwepo kwa muda mrefu, hasa katika maeneo ya Zanzibar na Nyanda za Juu Kusini. “Tunamtolea Ado tahadhari, akome mara moja, la sivyo tutaamua hatua za kuchukua,” walisisitiza na kuongeza,

“Tungependa kumkumbusha anachokijua Ndugu Ado kwamba CUF- Chama Cha Wananchi ni Chama imara chenye mizizi madhubuti ambayo hatoweza kuing’oa kwa kuongea mbele ya kipaza sauti kwamba ‘CUF imekufa’”.

Licha ya shinikizo kutoka CUF, Ado amesema ataendelea kuwashawishi wanachama wa CUF kujiunga na ACT-Wazalendo, akisema ni jukumu lake kama mwanasiasa kushawishi wanachama wa vyama vingine.

“Binafsi sitaacha kuwashawishi wanachama wa CUF kuja ACT Wazalendo kama ambavyo ninafanya kwa wanachama wa CCM, Chadema, wasio na vyama nk. Hiyo ndio kazi ya mwanasiasa. Badala ya kutoa matusi na vitisho, CUF pia wana wajibu wa kufanya hivyo”, ameeleza Ado.

Hali ya mgogoro kati ya vyama hivi inaonekana kuendelea kutokota, huku kila upande ukijizatiti kulinda maslahi yake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!