Latest Posts

MGOMBEA CCM AONYWA KUTUMIA JINA LA “MSUBHATI” LA CATHERINE

Kampuni ya mawakili ya Divina Attorneys imetoa notisi ya kisheria kwa mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Joseph, ikimtaka kuacha mara moja kutumia jina la kisiasa “Msubhati” ambalo inadai ni mali ya kisiasa ya mpinzani wake, Catherine Nyakao Ruge wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA).

Katika barua ya tarehe 12 Septemba 2025 ambayo Jambo TV imeiona, mawakili hao wamesema Ruge amekuwa akitambulika kwa jina la Msubhati kwa zaidi ya miaka saba na kwamba jina hilo limejijengea heshima, hadhi na utambulisho wa kisiasa unaojulikana kwa wapiga kura na wapinzani.

“Mteja wetu amepata sifa na utambulisho mkubwa hadharani kupitia jina Msubhati. Ni jina linalotambulika wazi na wapiga kura, wapinzani wa kisiasa na umma kwa jumla. Kutumia jina hilo bila ridhaa yake ni udanganyifu na kunaharibu heshima yake ya kisiasa,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Divina Attorneys imemtuhumu mgombea wa CCM kwa kutumia jina hilo katika kampeni zake na hata kujitangaza kama “Original Msubhati”, jambo ambalo wanasema linaweza kuleta mkanganyiko kwa wapiga kura na kuathiri haki ya mteja wao kisiasa.

Kupitia barua hiyo, Mary Daniel Joseph ametakiwa kuacha mara moja kutumia jina Msubhati katika kampeni, matangazo au mawasiliano yake ya kisiasa, kuwasilisha maandishi ya kukiri na kuthibitisha kuacha kutumia jina hilo kabla ya saa 8 mchana, Septemba 12, 2025, na kutozindua rasmi kampeni zake chini ya utambulisho huo.

Aidha, mawakili hao wameonya kwamba iwapo hatozingatia maagizo hayo, watamshitaki Mahakama Kuu ya Tanzania wakitaka zuio la kisheria, fidia ya uharibifu wa hadhi ya kisiasa na tamko la kuthibitisha kuwa jina Msubhati ni mali ya kisiasa ya Catherine Ruge.

Pia wametishia kupeleka malalamiko kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Kamati ya Maadili ya Uchaguzi wakitaka kuchukuliwa hatua za haraka na kinidhamu dhidi yake.

Barua hiyo inasisitiza kuwa hatua hizo zinachukuliwa “kwa uzito mkubwa” na kumtaka mgombea huyo wa CCM kupata ushauri wa kisheria endapo hatambui madhara ya notisi hiyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!