Latest Posts

MGONGANO WA KAULI KATI YA BAWACHA NA POLISI KUHUSU KESI YA LUCY SHAYO

Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Kanda ya Pwani limelaani hatua ya Polisi Mkoa wa Morogoro kumshikilia mwanachama wake, Lucy Shayo, kwa zaidi ya siku tatu bila dhamana, wakidai kitendo hicho ni kinyume cha sheria na haki za binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Septemba 13, 2025 iliyosainiwa na Mwenyekiti wa BAWACHA Kanda ya Pwani, Rose Moshi, Shayo alikamatwa Septemba 10 akiwa safarini kutoka Iringa kuelekea Dar es Salaam kuhudhuria kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

“Pamoja na kwamba shtaka linalomkabili ni la kusambaza taarifa za uongo na ni la dhamana, Polisi wamezuia dhamana yake na kuendelea kumshikilia kinyume cha sheria,” imesema taarifa hiyo.

BAWACHA imetaja kitendo hicho kuwa ni ukiukwaji wa misingi ya haki na demokrasia, na imelitaka Jeshi la Polisi kumuachia huru mara moja endapo ni kweli ana makosa, ili hatua za kisheria zifanyike mahakamani.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, SACP Alex Mkama, Septemba 14, 2025, limefafanua kuwa Shayo na mwenzake Steven Godwel, mtumishi wa serikali, wanashikiliwa kwa tuhuma za kuandaa na kusambaza taarifa za upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii, taarifa ambazo zinadaiwa kuleta taharuki miongoni mwa wananchi.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro lilifuata taratibu zote za kuwakama Bi. Lucy Shayo na Ndugu Godwel, na hakuna nguvu yoyote iliyotumika kama inavyodaiwa mitandaoni. Wote walikamatwa wakiwa wanaishi katika nyumba moja, na sababu kubwa ni kuchapisha taarifa za uongo kuhusu CCM kutumia magari ya jeshi katika kampeni,” imeeleza Polisi.

Kamanda Mkama amesema uchunguzi bado unaendelea na hatua stahiki zitachukuliwa mara utakapokamilika, huku akibainisha kuwa watuhumiwa wengine wanaohusiana na tuhuma hizo pia wanatafutwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!