Latest Posts

MGONGANO WA KIMASLAHI UNAVYOUTAFUNA UONGOZI WA TGNP

Katika kile ambacho kinaelezwa kuwa mgongano na mgogoro wa kugombea nafasi za juu za uongozi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), serikali imeingilia kati na kusitisha Mkutano Mkuu wa Wanachama wa TGNP uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 18 Oktoba 2024 ambapo ulilenga kwa kiasi kikubwa kujadili ajira ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo ambalo ni moja ya mashirika kongwe nchini yanayohusika na kutetea haki za binadamu ikiwamo haki za kijinsi.

Hatua hiyo imekuja baada ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama wa TGNP kuhusu mpasuko unaoendelea ndani ya shirika.

Katika barua rasmi iliyotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, siku ya Ijumaa Oktoba 18, Msajili Vickness Mayao ameagiza kusitishwa kwa Mkutano Mkuu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hofu ya vurugu zinazoweza kutokea kutokana na mgogoro huo. Barua hiyo, yenye kumbukumbu namba CEA.225/335/01A/121, imeeleza kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu endapo mkutano utaendelea kama ulivyopangwa, jambo linalotishia usalama wa wanachama na uhai wa shirika.

Msajili pia amewataka viongozi wa TGNP kufika katika ofisi za Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali siku ya Jumatatu, tarehe 28 Oktoba 2024, Jijini Dodoma kwa mazungumzo na kushauriana kuhusu njia za kutatua mgogoro huo. Viongozi wa shirika wanatakiwa kupeleka orodha ya wanachama hai pamoja na nakala ya Katiba ya shirika ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu.

Katika hatua nyingine, barua iliyotolewa na Gemma Akilimali, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, siku moja kabla ya mkutano huo (yaani Oktoba 17, 2024) uliokuwa umepangwa Oktoba 18, 2024, ilithibitisha kuwa Msajili ameshauri mkutano huo usifanyike kwa sasa kutokana na uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokaribia.

Aidha, mwenyekiti huyo alieleza kuwa Msajili ameagiza mkutano huo kusitishwa mpaka uchaguzi huo utakapomalizika. Hata hivyo baadhi ya wanachama walikuwa wanahofu ikiwa kweli Msajili alitoa taarifa hiyo kwani hakukuwa na barua rasmi kutoka kwa msajili kabla ya taarifa ya Msajili ya siku ya Ijumaa Oktoba 18, 2024 ambayo nayo ilikuwa ikitiliwa mashaka uhalali wake.

Jambo TV tulilazimika kutafuta ukweli wa taarifa za Msajili ambapo kupitia kwa maafisa mawasiliano wa Wizara, tulifanikiwa kufahamu kuwa barua hiyo ilikuwa ya Msajili, hata hivyo hatukuweza kupewa nafasi ya kuhoji zaidi juu ya manung’uniko ya baadhi ya wanachama kwa Msajili ikiwa kama kweli taarifa ya awali iliyotolewa na TGNP ilieleza mkutano huo kuahirishwa kutokana na zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Matukio na taarifa hizo ni kama zimeongeza mvutano zaidi ndani ya TGNP, ambapo kumekuwa na malalamiko ya wanachama kuhusu mchakato wa ajira ya Mkurugenzi mpya wa shirika hilo.

Kutokana na taarifa ambazo Jambo TV imezipata, wanachama kadhaa wamekuwa wakilalamikia jinsi ambavyo uongozi umeshindwa kusimamia mchakato huo kwa uwazi, jambo ambalo linazidisha mgawanyiko ndani ya shirika.

Imeelezwa kuwa wanachama hao wanahoji taarifa ambazo zimekuwa zikitoka ndani ya siku tatu mtawalia tangu Oktoba 16 mpaka Oktoba 18, 2024, kwamba taarifa hizo zinalenga kupiga danadana zoezi la kupata Mkurugenzi mpya.

Wanachama hao wanasema kuwa kabla ya taarifa ya Shirika lao kusitisha mkutano kwa kigezo cha kupewa maagizo na Msajili, wao kama wanachama hai wa TGNP waliandika barua kwenda kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP aliyetajwa kwa jina la Gemma Akilimali kuhusu kuwepo kwa “Mkutano Mkuu wa Dharura Kuhusu Mchakato wa Mabadiliko ya Uongozi wa TGNP Ijumaa tarehe 18.10.2024”, ukilenga kupokea na kujadili taarifa ya mchakato wa kutafuta Mkurugenzi Mpya kutoka kwa Bodi.

“Katiba yetu inaelekeza kwamba Mkutano Mkuu wa Dharura wa Wanachama unaweza kuitwa kwa akidi ya 2/3 baada ya kutoa taarifa siku tano (5) kabla. Tunakutaarifu kuwa akidi hiyo imetimia, na mkutano utafanyika siku ya Ijumaa tarehe 18.10.2024, saa nane mchana kwa njia ya mtandao na ana kwa ana katika ofisi za TGNP, Mabibo Dar es Salaam”, ilieleza taarifa ya barua hiyo iliyoandikwa tarehe 14 Oktoba, 2024 ambayo Jambo TV tulipata kuifahamu.

Imeelezwa kuwa siku moja kabla ya tarehe 16 Oktoba, Kikao cha Bodi ya TNGP kiliendeshwa ambacho kilidaiwa kujadili suala la Mkurugenzi huyo na maandalizi ya mkutano ujao, baada ya kikao hicho, tarehe 17 asubuhi ndipo ikatolewa taarifa kwa wanachama ya kuwepo kwa mkutano huo na baadaye mchana siku hiyo, taarifa ya kusitishwa kwa mkutano huo ikatolewa ikielezwa kuwa ni maelekezo ya simu ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambapo wanachama wakaanza kuingiwa na hofu juu ya zoezi lao.

MGOGORO HUO KULIKONI?

Chanzo cha mgogoro huo ni mchakato wa ajira ya Mkurugenzi mpya wa TGNP, ambao unadaiwa kutawaliwa na hila na ushawishi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa juu wa shirika.

Tulipomtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi kuhusu sakata hilo, hakuwa na mengi ya kuzungumza isipokuwa akatuambia tumtafute Mwenyekiti wa Bodi Gemma Akilimali ambaye alipatikana na akithibitisha kuitisha mkutano wa bodi, mkutano wa kujadili ajira ya Mkurugenzi na kutoa taarifa ya kusitishwa mkutano huo lakini hakujibu kwanini hakukuwa na taarifa rasmi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa siku hiyo.

Vyanzo vingine kutoka ndani ya shirika vinaeleza kwamba kumekuwa na makundi ambayo yamekuwa na ushawishi juu ya viongozi wa shirika na hivyo kusababisha mgawanyiko. Katika makundi hayo, kuna wanachama wanaoamini kwamba kuna wanachama wanaotaka kujimilikisha shirika kwa kuweka mtu wanayemtaka. Hali hii ndio iliyosababisha Msajili uingilia kati ili kunusuru shirika hili, huenda iknaashiria kwamba TGNP inakabiliwa na mgogoro wa ndani ambao umekuja kufichuka hadharani, huku serikali ikiingilia kati kutafuta suluhisho la kudumu.

Wanachama wa TGNP wanatarajiwa kutumia muda uliobaki kutafakari masuala yanayopelekea mgawanyiko na kujiandaa kwa ajili ya mkutano wa Dodoma kati yao na Msajili utakaotoa mwelekeo mpya kwa shirika hilo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!