Mtafiti wa masuala ya fedha katika Ubalozi wa Tanzania nchini Oman, Hashimu Mnubi, amepongeza hatua mbalimbali ambazo zimeimarisha uchumi wa Tanzania na kuipa shilingi ya Tanzania uthabiti dhidi ya Dola ya Marekani.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchi, Mnubi amebainisha mambo makuu matatu yaliyochangia mafanikio hayo: ongezeko la mauzo ya bidhaa nje, kuimarika kwa utalii na uwekezaji, na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na uchumi.
Akifafanua kuhusu mauzo ya bidhaa nje, Mnubi amesema kuwa bidhaa kama mazao ya kilimo na dhahabu zimechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la mapato ya fedha za kigeni.
Amesema, “Over the past months kumekuwa na ratio kubwa sana ya mauzo ya bidhaa zetu nje, ama huduma, mali ghafi au processed, ambazo zimetupa hii stability tunayoiona leo. Mazao kama korosho na avocado pamoja na dhahabu vimetubeba sana.”
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), katika mwaka ulioishia Julai 2024, mauzo ya nje ya huduma na bidhaa yalifikia Shilingi trilioni 34, huku ukuaji mkubwa wa sekta hii ukichangia uthabiti wa Shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Mnubi pia amezungumzia mchango wa utalii na uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI). Amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya utalii huku uwekezaji ukiongezeka kwa kasi. Kwa mujibu wa taarifa za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024, Tanzania ilipokea uwekezaji wa dola bilioni 1.6, ongezeko la asilimia 53 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita. Mnubi ameeleza kuwa mafanikio haya si bahati mbaya, bali ni matokeo ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wa sera za fedha, Mnubi ameipongeza BoT kwa kusimamia mzunguko wa fedha na kudhibiti kiwango cha mfumuko wa bei (inflation). Tanzania imeweza kudumisha kiwango cha mfumuko wa bei katika wastani wa asilimia 3-5, hatua ambayo imesaidia kuimarisha uchumi.
Amesema, “Benki Kuu ya Tanzania inabeba maua yao kwa kuweka sera madhubuti ambazo zimewezesha ustawi wa shilingi na uthabiti wa uchumi.”
Mnubi amehitimisha kwa kusisitiza kuwa hatua hizi za kiuchumi zinaonesha kuwa Tanzania iko katika mwelekeo sahihi wa maendeleo, huku akiipongeza serikali kwa jitihada zake za kufanikisha ukuaji endelevu wa uchumi.