Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid inaendelea kupenya mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, na leo imewasili kwa wakazi wa Kata ya Manzese, Manispaa ya Ubungo, ambako wananchi wamepatiwa elimu juu ya masuala ya fedha na mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kukopa.
Katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Scholastica Mality kutoka Wizara ya Katiba na Sheria alihutubia wananchi na kutoa tahadhari kuhusu mikopo isiyo salama.
“Katika siku ya leo tupo katika kata hii ya Manzese, na banda letu kwa wale wanaohitaji msaada zaidi lipo katika Mtaa wa Mnazi Mmoja. Mnakaribishwa mkishatoka hapa kwa Mheshimiwa,” alisema Mality.
Akiwaelimisha wananchi, Mality alisisitiza umuhimu wa kufahamu masharti ya mkopo kabla ya kuuchukua na kuhakikisha mkopeshaji ni halali na amesajiliwa kisheria.
“Naomba tufahamu, wa kina mama, kina baba na kina kaka — mnapotaka kuchukua mkopo, fahamu unachukua mkopo wapi na fahamu yule atakayekupa mkopo kama amesajiliwa kufanya biashara hiyo ya kutoa mikopo,” alieleza.
Aliwahimiza wananchi kuwa na malengo ya wazi kabla ya kukopa na kutathmini uwezo wao wa kuurejesha mkopo.
“Jambo la kwanza la kuzingatia ni kujua mkopo huo unauchukua kwa ajili ya jambo gani, lakini pia fahamu utaweza kuurejesha kwa namna gani. Jambo jingine muhimu sana ni mkataba wa mkopo. Usichukue mkopo bila mkataba,” alisisitiza.
Mality aliwakumbusha wakazi wa Manzese kuwa mkataba wa mkopo ndiyo msingi wa ulinzi wa kisheria, hivyo lazima usomwe kwa makini kabla ya kusainiwa.
“Ule mkataba usome vizuri, ndiyo unatambulika kisheria. Unapochukua mkopo, anayekupa mkopo aonekane kwenye mkataba, anakupa kiasi gani kionekane, namna ya marejesho, kiwango cha riba na aina ya dhamana — vyote viwe kwenye mkataba.
Usiweke sahihi yako kama hujausoma huo mkataba, kwa sababu kwa mujibu wa sheria, unapoweka sahihi umekubaliana na yale yote yaliyoandikwa katika mkataba ule,” aliongeza.
Kampeni ya Mama Samia Legal Aid inaendelea kuwa msaada mkubwa kwa wananchi hasa wa kipato cha chini, kwa kuwapa elimu ya kisheria ili kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi na kujilinda dhidi ya mikopo kandamizi