Latest Posts

MIKOPO UMIZA YAVURUGA MAISHA YA WANAWAKE, ADC YATOA ONYO

Wanawake wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) Mkoa wa Mwanza wamepaza sauti dhidi ya mikopo kandamizi maarufu kama kausha damu, wakiiomba Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kusaidia wananchi wenye kipato cha chini kupata mikopo salama na yenye masharti nafuu.

Katika kongamano la wanawake na wajasiriamali lililoandaliwa, Machi 25, 2025, na Chama cha ADC, Halima Mfaume, Katibu wa Wanawake wa chama hicho mkoani Mwanza, amesimulia changamoto alizopitia baada ya kudhamini mkopo kwa mtu aliyekimbia deni, hali iliyomsababishia fedheha na usumbufu mkubwa.

“Nilisumbuana nao mpaka kwa Mwenyekiti wa mtaa, nikadhalilika mtaani kana kwamba mimi ndiye nimekopa. Hali hii ilinifanya nitamani siku moja wanawake tupaze sauti zetu dhidi ya mikopo hii ya dhuluma,” amesema Halima.

Akiendelea kusimulia, amesema kuwa watu wa kausha damu hawana heshima kwa wateja wao na hufanya vitendo vya udhalilishaji wanapodai fedha zao.

“Nilipata ujumbe kwamba kuna watu walifika nyumbani kwangu, ilipofika jioni wakaja tena. Walifika bila kugonga mlango, wakapitiliza ndani na kunitaka nirejeshe mkopo wa Sh150,000 niliodhamini, kwani aliyekopa haonekani,” amesema.

Kutokana na changamoto hizi, Halima ameishauri Serikali kuweka mikopo midogo inayoanzia Sh100,000 na kuendelea, ili kusaidia wananchi wenye kipato cha chini kukopa kwa usalama badala ya kutegemea kausha damu.

Amesema kuwa licha ya Serikali kutoa mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri, taratibu za kuipata ni ngumu na zimejaa urasimu.

“Mikopo hii inaweza kuchukua hadi miezi mitatu kupatikana, na kuna vikwazo vingi, ikiwa ni pamoja na kutakiwa kupata sahihi ya Mwanasheria Mkuu, hali inayowafanya watu kukata tamaa na kuingia kwenye mikopo hatari,” ameongeza.

Mkazi wa Nyashana, Jesca Enock, ameiomba Serikali kuwekeza kwenye utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kukopa kutoka kwenye taasisi rasmi za fedha ili kuepuka mikopo ya riba kubwa na masharti kandamizi.

“Tatizo kubwa ni ukosefu wa elimu. Kama tutaelimishwa kuhusu mikopo salama, tutakopa kwenye taasisi rasmi na kuachana na mikopo ya kihuni,” amesema Jesca.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Katibu wa Wanawake ADC Taifa, Sarah Joseph, amesema kuwa mikopo ya dhuluma imechangia kuvunjika kwa ndoa nyingi na kuwatumbukiza wanawake katika matatizo makubwa ya kifamilia.

“Baadhi ya wanawake wameachika, wengine wanahangaika kulea watoto peke yao, na wengine wamekimbia ndoa zao kwa sababu ya madeni ya mikopo umiza,” amesema.

Sarah pia amedai kuwa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya bajeti ya Halmashauri umejaa ubaguzi wa kisiasa, hali inayowafanya wananchi wengi kushindwa kunufaika nayo.

“Mikopo hii inatolewa kwa misingi ya upendeleo. Kama si mwanachama wa chama kilicho madarakani, hupati mkopo, hata ukiwa na sifa zote,” amesisitiza.

Mgeni rasmi wa kongamano hilo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shaban Itutu, amewataka wananchi kuungana kwa pamoja kupambana na mfumo wa mikopo kandamizi.

“Maisha haya yanahitaji mtu kuwa na uchungu na hali yake. ADC inalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kujikwamua kiuchumi,” amesema Itutu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!