Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeeleza kupata mafanikio makubwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, likibainisha malengo ya faida ya TZS bilioni 28.6 kabla ya kodi lakini limevuka malengo haya kwa kupata faida ya Sh bilioni 42.8, ikiwa ni asilimia 168.6 zaidi ya lengo lililowekwa.
Uwezo huu wa kifedha unaonesha maendeleo makubwa katika usimamizi wa mapato na matumizi ya shirika. Katika mwaka huu, mchango wa NHC kwa pato la taifa kupitia kodi umefikia kiasi cha Shilingi bilioni 30.24. Hii inaashiria mchango mkubwa wa shirika katika mfuko wa hazina na pia inaonesha jinsi NHC inavyosaidia katika kuimarisha uchumi wa nchi kupitia mchango wake wa kodi.
Miradi muhimu inayosimamiwa na NHC inaendelea vizuri ikiwamo mradi wa Morocco Square ambao tayari uuzaji wa nyumba 72 kati ya 100 umefanyika, eneo la maduka ya biashara asilimia 98 likiwa limepangwa, na nusu ya maeneo ya ofisi ndani ya mradi wa Morocco Square nayo yamechukuliwa.
Mradi wa Kawe 711, ujenzi wake umefikia asilimia 45, ukitarajiwa kukamilika Aprili 2026, Samia Housing Scheme; Ujenzi wa nyumba 560 Dar es Salaam umefikia asilimia 65 kufikia Julai 2024 na Iyumbu ambapo mradi umekamilika kwa asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Septemba 2024.
Maalumu kabisa mradi wa makazi wa Samia unaofahamika kama ‘Samia Housing Scheme’, umelenga kujenga nyumba (units) 5,000 za kipato cha kati katika mikoa mbalimbali nchini. Mradi huu unaokadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 466, utakamilishwa kwa awamu katika maeneo mbalimbali nchini na Dar es Salaam pekee utatekelezwa kwa asilimia 50 ya nyumba hizo 5000.
Aidha NHC ina miradi ya Ukandarasi na Ushauri ikiwamo wa Mji wa Serikali Mtumba ambao ujenzi wake umefikia asilimia 85 na umepatiwa muda hadi Septemba 30, 2024, jengo la uchumi la UDSM ambalo limefikia asilimia 78, Taasisi ya Moyo ya JKCI asilimia 99, na Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Nyerere asilimia 100 iliyopo Kwangwa, Musoma, umekamilika kwa asilimia 100.
Katika maendeleo ya majengo ya biashara, NHC imeanzisha ujenzi katika maeneo kama Kahama (asilimia 20) na imeanza maandalizi ya ujenzi Masasi na Mtanda- Lindi. Ujenzi wa majengo ya biashara huko Kahama umefikia asilimia 20 na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu. Kadhalika, maandalizi ya ujenzi wa majengo ya biashara Masasi na Lindi yamekamilika, na ujenzi umeanza Julai 2024.
NHC ina mipango ya kufanya mambo makubwa zaidi katika sekta ya makazi, ikiwemo kurejesha miradi iliyokwama na kukabiliana na mahitaji ya ongezeko la watu. Shirika linajitahidi kuongeza juhudi katika kuhakikisha watanzania wanapata makazi bora na endelevu.
Taarifa hizi zinaonesha jinsi NHC inavyokuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya miundombinu ya makazi nchini Tanzania na jinsi inavyoweza kufanikisha malengo yake kwa ufanisi.