Kuelekea Uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi CCM wametakiwa kuweka tofauti zao pembeni na badala yake wawe kitu kimoja ili waweze kuweka msingi imara kwa wenyeviti wa serikali za mitaa.
Hayo ameyazungumza na Mjumbe wa Halmashauri Kuu wilaya ya Mtwara Mjini, Engetraud Mbemba Septemba 17,2024 kwenye kikao cha Kamati ya Siasa kilichofanyika mtaa wa Ligula tawi la Mbelenje Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Aidha amewataka wanachama hao kuungana kwa pamoja ili kujenga safu nzuri kuanzia chini hadi itakapofika uchaguzi mkuu utakao fanyika 2025 wa kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani kusiwe na mashaka.
“Tuondoe tofauti zetu tuchague chama cha mapinduzi kwasababu maendeleo yanatoka kwenye mitaa, mwenyekiti wa mtaa ana wajumbe wake kukiwa na tatizo utaanza kwa mwenyekiti huwezi moja kwa moja ukaenda kwa mbunge, unatakiwa kuchagua mwenyekiti ambae anakubalika ili wenzetu wakija kusiwe tena na msuguano wa mashaka na mwenyekiti mliomchagua.”Amesema Mbemba
Ameongeza kuwa mtaji wa ushindi ni kuwa na wanachama wengi na sio malumbano kwani uwepo wa wanachama wengi ndio utakaopelekea ushindi hivyo wajitokeze kwa wingi kwenye zoezi la kuhakiki kadi ili waweze kupata wanachama wengi ambao watakwenda kupiga kura.
Mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini Hassan Mtenga ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu wilaya ya Mtwara mjini amewataka viongozi wa chama hicho kuacha ugomvi usio kuwa na lazima na badala yake waishi kwa kutegemeana kwa kila mmoja kuzingatia mipaka yake ili kuzidi kuleta maendeleo kwenye chama.
Sambamba na hilo amesema atazunguka kila tawi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanachama wa CCM ili kufanya maandalizi kuelekea uchaguzi huo na kuhakikisha wanapata ushindi katika mitaa yote.
Naye Diwani wa kata ya Shangani Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, Abuu Mohamed ametoa rai kwa wanachama kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kudumu ili kila mwanachama aweze kupata haki ya kupiga kura mana hakuna haki bila ya kuwa na wajibu.