Latest Posts

MKATABA ULIVUNJWA KINYUME CHA SHERIA: WAPANGAJI WADAI FIDIA YA MILIONI 100

Kutokana na shauri lililodumu kwa zaidi ya miaka mitano katika Baraza la ardhi na Nyumba la Wilaya ya Dodoma Mjini, hatimaye limetolewa uamuzi wake ambapo baraza hilo limewataka waliokuwa wapangaji wa maduka kwenye nyumba namba 10 kitalu M iliyopo mtaa wa Uhindini Jijini Dodoma kufungua kesi ya madai kwenye mahakama zinazohusika kwani baraza hilo halina mamlaka ya kusikiliza kesi za jinai.

Akisoma hukumu hiyo Ijumaa Januari 24, 2025 Mwenyekiti wa baraza hilo Omar Mbega amesema waleta maombi kwenye baraza hilo ambao walikuwa wapangaji wa maduka kwenye nyumba iliyouzwa na mali zao kuchukuliwa kusikojulikana na aliyenunua nyumba hiyo bila kuzingatia haki zao za kisheria.

Waleta maombi kwenye shauri hilo namba 240 la mwaka 2019 ni Nadya Abdallah na Waziri Kivale ambao walikuwa ni wapangaji wa maduka kwenye nyumba hiyo ya Mohamed Maddar ambaye aliiuza kwa Chef Asili Company Limited bila kuzingatia matakwa ya kisheria ya mikataba wa upangaji.

Waleta maombi hao waliwakilishwa na Wakili Marco Kisakali ambapo walisema kuwa mikataba wao wa upangaji wa maduka ulivunjwa bila kufuata utaratibu wa kisheria wala kuzingatia kuwa walikuwa bado hawajamaliza mkataba wao.

Aidha wamesema kuwa hawakutaarifiwa kuwa nyumba hiyo imeuzwa na badala yake aliyenunua nyumba hiyo alivunja maduka yao na kutupa bidhaa zilizokuwepo nje na kusababisha uharibifu mkubwa.

“Wateja wangu hawakutaarifiwa kuwa nyumba hiyo imeuzwa na badala yake walikuta maduka yao yamevunjwa na bidhaa zao zimetupwa nje na mpaka sasa hazijulikani zilipo na wakati walikuwa na mkataba hai wa kuendelea kufanya biashara kwenye maduka hayo,” amesema Kisakali.

Kisakali amesema wateja wake wamepata hasara ya bidhaa zao zaidi ya Shilingi milioni 100 kutokana na kusitishiwa mkataba na upotevu wa mali zao hivyo wanahitaji kulipwa fidia ikiwa ni pamoja na nafuu ya kuendesha kesi hiyo kwenye Baraza la Ardhi la Wilaya.

Akisoma hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Dodoma Mjini, Omar Mbega amesema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo unaonesha kuwa ni kweli wapangaji hao walikuwa na mkataba hai ambao ulivunjwa bila kufuata taratibu za kisheria kwani wapangaji hao walikuwa wamelipa kodi ya mwaka mzima wa 2019 na mkataba huo ulivunjwa Juni 17, 2019 bila makubaliano.

Aidha amesema pia ushahidi umeonesha kuwa wapangaji hao hawakurudishiwa pesa zao za kodi walizokuwa wamelipa kwa miezi iliyokuwa imebakia.

“Hatuwezi kusema kuwa hakuna hasara katika tukio hilo, kuna hasara kubwa kwa sababu maduka yamevunjwa ndani ya mkataba na mali zimepotea hivyo kuna hasara ambayo imepatikana,” amesema Mbega.

Amesema ushahidi uliotolewa na mjibu maombi namba mbili ambaye ni Chef Asili amesema kuwa mjibu maombi wa kwanza ambaye ndiye aliyemuuzia nyumba hiyo alimwambia kuwa atawalipa wapangaji kodi ya miezi iliyobakia lakini hakufanya hivyo.

Ameeleza pia mjibu maombi namba mbili ambaye ni Chef Asili alisema kuwa alipofika kwenye nyumba hiyo alikuta maduka yamefungwa na bidhaa zipo nje hivyo aliamua kwenda kuzihifadhi hali inayodhihirisha kuwa alihusika kwenye uvunjaji wa maduka hayo.

“Kwa sababu haiwezekani kama huhusiki na uvunjaji wa maduka uhusike kwenye kuhifadhi mali ambazo huwajui wahusika huu ni wizi, na hili ni kosa la jinai la kuvunja na kuchukua mali ambayo siyo yako, kwa hiyo naomba mwende kwenye mahakama zinazosikiliza makosa ya jinai kwa sababu hii mahakama haina mamlaka hayo,” amesema Mbega.

Amesema kuhusu kuvunjwa mkataba wa upangaji pia kuna mahakama ambazo zinasikiliza mashauri hayo hivyo wanatakiwa kwenda kufungua mashauri huko, ya madai ya kuvunjiwa mkataba.

Amesema mahakama hiyo ya ardhi ina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya mikataba ya ardhi na nyumba na si kusikiliza mashauri ya jinai.

Pia kuhusu nafuu ya gharama za uendeshaji wa kesi hiyo kwa miaka mitano mitano amesema kwakuwa hakuna aliyeshinda kesi hiyo hakuna atakayelipa gharama hizo na kwamba nafasi ya kukata rufaa kwenda mahakama kuu iko wazi kwa wale ambao hawajaridhika na uamuzi huo.

Akizungumza nje ya mahakama wakili wa waleta maombi amesema wanasubiri nakala ya hukumu itoke ili wajue cha kufanya baada ya kushauriana na wateja wake.

Wapangaji hao wawili walivunjiwa maduka na bidhaa zao kutupwa nje baada ya nyumba waliyokuwa wamepanga kuuzwa kwa mtu mwingine na mkataba wao wa kupanga nyumba hiyo kuvunjwa bila kufuata utaratibu wa kisheria Juni 2019 na wakati mkataba wao ulikuwa unamalizika Disemba 31, 2019.

Katika shauri hilo Chef Asili aliwakilishwa na mawakili kutoka Njulumi and Company Advocate na mjibu maombi namba moja hakutokea mahakamani hata mara moja hivyo hukumu ilisomwa bila uwepo wake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!