Na Josea Sinkala, Chunya Mbeya.
Halmashauri ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya imetoa mkopo wa shilingi Billion 1.8 kwa vikundi vya wajasiriamali na wafanyabiasha zaidi ya mia moja katika wilaya ya Chunya na kuwataka wanufaika kuzingatia suala la uaminifu wa kurejesha mikopo hiyo.
Mikopo hiyo imetolewa kwa mujibu wa takwa la kisheria kuhakikisha kila Halmashauri kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani ili kuzikopesha kwa makundi ya wanawake (asilimia nne), vijana (asilimia nne) na wenye ulemavu (asilimia mbili) ambapo makundi hayo yote matatu kwa wilaya ya Chunya yamenufaika kupitia mikopo hiyo.
Afisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya wilaya ya Chunya Bi. Marietha Mlozi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Tamim Kambona, amesema pamoja na changamoto kwa baadhi ya watu kutokuwa waaminifu kwenye urejeshaji mikopo hiyo lakini bado wanaendelea kuwaelimisha wananchi na kutoa mikopo hiyo ili kuhakikisha wananchi wanajiimarisha kiuchumi na kuinua uchumi wa taifa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wilaya ya Chunya, Ezelina Mwakisole na Katibu wa Jumuiya ya Vijana UVCCM wilaya ya Chunya wameishukuru Serikali kwa kuendelea kusimamia utolewaji mikopo hiyo na kuwataka wanufaika kuwa waaminifu ili kuboresha mitaji ya biashara na shughuli zao mbalimbali wanazozifanya.
Akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya zaidi ya shilingi billion 1, Mbunge wa jimbo la Lupa Masache Kasaka, amewaasa wananchi waliopata mikopo hiyo ya bila riba kutumia kwa nidhamu fedha hizo na kuimarisha uchumi wao, vikundi na jamii kwa ujumla.
Masache amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kutoa mikopo hiyo ikiwa ni sehemu ya kurejesha makusanyo ya mapato kwa wananchi ili kuhakikisha wanajiendesha hasa kiuchumi.
Baadhi ya wananchi walionufaika na mkopo huo usio na riba wamesema watakuwa waaminifu wa kurejesha mikopo hiyo na kuhakikisha wanaboresha miradi yao na kujiinua kiuchumi.