Serikali imeanza maandalizi ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI 2), ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji nchini kwa miongo ijayo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, siku ya Ijumaa Juni 6, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, amesema maandalizi ya awali yamekamilika na sasa kamati ya maandalizi inakwenda kuanza hatua ya pili ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau katika mikoa 16 ya Tanzania Bara.
“Lengo ni kuhakikisha tunapata maoni mapana kutoka kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa, wawekezaji wa ndani na nje, wananchi wa kawaida, sekta binafsi na ya umma, ili mpango huu uweze kujibu matarajio ya Watanzania na kusaidia uchumi wetu kukua,” amesema Prof. Mkumbo.
Waziri huyo amekumbusha kuwa mpango wa awali (MKUMBI 1) ulianza mwaka 2018 na umeleta mafanikio pamoja na kubainisha changamoto mbalimbali. Hivyo, MKUMBI 2 umelenga kupitia upya mazingira ya sasa ya biashara na uwekezaji ili kuweka mikakati bora zaidi kwa miongo ijayo, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa mujibu wa Waziri, timu ya maandalizi iliyo chini ya Prof. Faustin Kamuzora, sasa itaelekea mikoani kuzungumza na wadau na kukusanya maoni yao kuanzia Juni 15, 2025, ambapo mchakato utaanza na hatua ya majaribio (pilot phase) kabla ya kusambaa nchi nzima.
“Tutaanza na maswali ya majaribio ili kujiridhisha kama yanakidhi viwango, kisha tutatawanyika kwenye kanda mbalimbali. Mikoa yote itashiriki, na tutatumia njia za ana kwa ana pamoja na njia za kidijiti kuhakikisha tunawafikia wadau wengi iwezekanavyo,” amesema Prof. Kamuzora.
Kamati hiyo pia inafanya kazi kwa karibu na tume ya kitaifa iliyoundwa na Rais kwa ajili ya kupitia mfumo wa kodi nchini, ambao umetajwa kuwa ni sehemu muhimu ya mazingira ya biashara.
Prof. Kamuzora amesema baadhi ya maeneo mapya yatakayozingatiwa katika MKUMBI 2 ni pamoja na kuibuka kwa biashara mpya kama startups (biashara change) na biashara za mtandaoni ambazo hazikupewa uzito mkubwa katika MKUMBI 1. Pia amesema kuwa biashara ndogo ndogo kama za kina mama ntilie, ambazo zinahusisha idadi kubwa ya wananchi, sasa zitapewa kipaumbele katika ukusanyaji wa maoni na uboreshaji wa mazingira yao.
“Takwimu zinaonesha watu wengi wanafanya biashara ndogo ndogo. Tutaenda kuwasikiliza na kuona serikali ifanye nini ili mazingira yao yawe bora zaidi,” ameeleza Prof. Kamuzora.
Waziri Mkumbo ametoa wito kwa vyama vya wafanyabiashara, wawekezaji, na taasisi mbalimbali mikoani kujiandaa kuwapokea wajumbe wa kamati na kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mpango huu unakuwa shirikishi na unaolenga maendeleo ya taifa.