Latest Posts

MKURUGENZI AMSONS: KAMPUNI ZA KICHINA NI TISHIO KUBWA AFRIKA MASHARIKI

Katika juhudi za kujitanua kwenye sekta ya saruji Afrika Mashariki, Amsons Group ya Tanzania inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa kampuni kubwa za Kichina zenye mtaji mkubwa na kiu ya upanuzi, anasema Edha Nahdi, Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons akizungumza na The Africa Report.

Mnamo 2024, Amsons Group ilianzisha mchakato wa kuinunua Bamburi Cement kwa TZS 500 bilioni ($182 milioni). Ingawa Holcim, mmiliki wa asilimia 58.6 ya Bamburi, ilikubali awali kuuza hisa zake kwa Amsons, baadaye ilijiondoa katika mpango huo, jambo lililofungua upya mchakato wa ununuzi.

“Kulikuwa na ushindani mkubwa,” anasema Nahdi. ” Kampuni kutoka Afrika Kaskazini, India na China zilivutiwa na ununuzi huu, hivyo mchakato wa zabuni ulikuwa mkali sana. Tulilazimika kujitoa kifedha ili kufanikisha mpango huu.”

Hatimaye, mashindano ya ununuzi yalibakia kati ya Savannah Cement ya Kenya na Amsons. Hata hivyo, baada ya Savannah Cement kupendekeza ununuzi wa Bamburi kwa TZS 550 bilioni ($214 milioni), mmiliki wake, Benson Ndeta, alikamatwa kwa tuhuma za udanganyifu, na hivyo kampuni hiyo kujiondoa kwenye mpango wa ununuzi.

Vyombo vya habari vya Kenya viliripoti wakati huo kwamba utetezi wa Ndeta ulidai kuwa kukamatwa kwake kulikuwa njama ya kuizuia Savannah kushinda zabuni ya Bamburi. Uuzaji wa hisa za Bamburi katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE) ulisitishwa kuanzia Februari 27 hadi Mei 9, kabla ya mpango wa kuiondoa sokoni

Baada ya mpango wa ununuzi kukamilika kufikia katikati ya Mei, Nahdi anasema wanapanga kuiorodhesha Bamburi Cement upya kwenye Soko la Hisa la Nairobi (NSE).

“Kwa upanuzi wetu, tutaingia kwenye soko kwa kiwango kikubwa zaidi,” anasema Nahdi.

Amsons ilianza safari yake ya upanuzi mwaka 2023 kwa kununua asilimia 65 ya Mbeya Cement kutoka Holcim Group, kampuni mama ya Lafarge, kwa takriban TZS 444 bilioni ($175 milioni). Ununuzi huo uliwapa fununu kuwa Lafarge ilikuwa na mpango wa kujitoa kikamilifu katika soko la Afrika Mashariki, jambo lililowafanya kuwa tayari kwa mpango wa Bamburi.

Amsons ilitumia takriban miaka miwili kufanya uchambuzi wa soko kabla ya mpango wa Bamburi, anasema Nahdi. Hatua hiyo ya awali iliiweka kampuni hiyo katika nafasi bora zaidi kuliko washindani wake ambao walikuwa bado wanajiandaa wakati Amsons ilikuwa tayari kuchukua hatua. Anaeleza kuwa mchakato wa kina wa tathmini ya ununuzi ulitoa nafasi ya kushinda Bamburi licha ya ushindani mkali – na wanapanga kutumia mbinu hiyo hiyo kwa manunuzi mengine katika ukanda huu.

Katika hatua ya kusukuma mbele ajenda yake ya kuwa mtayarishaji mkuu wa saruji Afrika Mashariki, Amsons inatarajia kuwekeza TZS 812 bilioni ($320 milioni) kuboresha kitengo cha uzalishaji wa klinka cha Bamburi kilichopo Mombasa. Kazi ya ujenzi inatarajiwa kuanza Oktoba, huku uzalishaji ukitarajiwa kuanza ndani ya miezi 24. Mbali na Mombasa, kampuni hiyo pia inapanga kufungua viwanda viwili vipya vya saruji nchini Tanzania.

Vilevile, Amsons inatafuta fursa nchini Uganda. Mnamo Machi 2024, Bamburi Cement ilikamilisha uuzaji wa hisa zake 70% katika kampuni yake tanzu ya Uganda, Hima Cement, kwa Sarrai Group na Rwimi Holding kwa thamani ya takribani $84 milioni (TZS 214 bilioni).

“Uganda ni ndugu wa Kenya na Tanzania. Tunaunganishwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kuna fursa nyingi za uwekezaji, iwe kupitia ununuzi wa kampuni au miradi mipya,” anasema Nahdi.

Licha ya mafanikio haya, Amsons inakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa kampuni kubwa za Kichina kama Huaxin Cement, Sinoma Cement, na West International Holding, ambayo yamewekeza mabilioni ya dola katika sekta ya saruji barani Afrika.

“Kampuni za Kichina ni tishio kubwa kwa ukanda huu kutokana na uwekezaji wao mkubwa na miradi yao mipya,” anasema Nahdi.

“Kwa kampuni za China, dili kama hili ni kama ‘pesa ya kuchezea’ (Mickey Mouse money). Ninaamini kuwa kampuni za ndani zinapaswa kusimama imara dhidi ya ushindani kutoka China na kutafuta mbinu tofauti za kukua. Huenda tukishirikiana tutakuwa na nafasi bora zaidi,” anaongeza.

Ushindani wa muda mrefu kati ya Tanzania na Kenya, unaohusisha siasa, biashara, michezo na utalii umeathiri kwa kiwango fulani mchakato wa kuiunganisha Afrika Mashariki, na kufanya nchi hizo mbili zisionekane kama washirika wa kibiashara wa moja kwa moja.

Mizozo ya mara kwa mara kuhusu vikwazo visivyo vya ushuru kati ya Kenya na Tanzania imekuwa ikizuka na kupoa kwa miaka mingi. Mapema mwaka 2024, Mamlaka ya Kilimo na Chakula ya Kenya (AFA) ilianzisha tozo ya 2% kwa nafaka na kunde, hali iliyosababisha malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa Tanzania na kusababisha kuzuiwa kwa zaidi ya malori 40 katika mpaka wa Namanga.

“Baadhi ya watu wanafikiri kuwa Tanzania na Kenya ni washindani wakubwa, lakini si kweli. Mabenki ya Kenya kama KCB na Equity yamekuwa yakifanya kazi Tanzania kwa miaka 14 au 15 kwa mafanikio makubwa,” anasema, hata hivyo, anataja kuwa Kenya ina uchumi ulioendelea zaidi, huku Tanzania ikiwa katika hatua ya ukuaji wa kasi.

“Hii inamaanisha kuna fursa nyingi za kipekee kwa sekta tofauti katika kila nchi. Lakini kama mataifa jirani, sisi si washindani sisi ni washirika wa maendeleo,” anasisitiza Nahdi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!