Manusura wa mkanyagano mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini India kwa zaidi ya muongo mmoja bado wameendelea kufuatia tukio la mkusanyiko wa kidini wa Kihindu wa siku ya Jumanne Julai 2, 2024 uliojaa msongamano mkubwa na kusababisha vifo vya watu 121.
Kulingana na Shirika la habari la AFP, ripoti ya polisi imesema zaidi ya watu 250,000 walihudhuria hafla hiyo katika jimbo la Uttar Pradesh Kaskazini mwa India, mara tatu zaidi ya wale walioruhusiwa na waandaaji, ambao walikuwa 80,000.
“Watu walikuwa wakiangukiana juu ya mteremko ulioelekea kwenye mtaro uliojaa maji” Walioshuhudia walisema.
Afisa Polisi ambaye alikuwa zamu Jumanne wakati ambao mhubiri maarufu wa Kihindu akitoa mahubiri, Sheela Maurya (50) alisema kuwa watu katika umati wakiwamo wanawake na watoto waliondoka eneo la tukio mara moja. Hata hivyo wengi wa waliokufa ni wanawake, pamoja na watoto saba na mwanaume mmoja.
Maafisa wameeleza kuwa mkanyangano huo ulisababishwa na waumini waliokuwa wakijaribu kukusanya udongo kutoka kwenye nyayo za mhubiri huyo huku wengine wakisema sababu ni dhoruba ya vumbi kuzua hofu.
Kwa mujibu wa Kituo cha habari cha India cha Mirror Now, mkusanyiko huo ulisababisha baadhi ya watu kuzirai kutokana na nguvu ya umati, kabla ya kuanguka na kukanyagwa kwa kushindwa kusonga mbele.
Alfajiri ya Jumatano Julai 03, 2024 maiti nne ambazo hazijatambuliwa zililala kwenye ghorofa ya chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali iliyo karibu na mji wa Hathras wakati ambao baadhi ya raia wakiwatafuta ndugu zao waliopotea, wakiwa hawafahamu kama wangali wazima au wameshatangua mbele ya haki.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ametangaza fidia ya dola 2,400 kwa ndugu wa karibu wa waliofariki na dola 600 kwa wale waliojeruhiwa katika tukio hilo huku Rais wa India Droupadi Murmu akieleza vifo hivyo kuwa vya kuhuzunisha na kutoa salamu zake za rambirambi kwa jamaa wa wafiwa.
Kituo cha habari cha ABP LIVE kimesema kuwa Waziri Mkuu wa jimbo la Uttar Pradesh, Yogi Adityanath ambaye pia ni mtawa wa Kihindu alitoa rambirambi zake kwa jamaa za waliouawa na kuamuru uchunguzi wa vifo hivyo.
Mikusanyiko ya kidini nchini India ina rekodi mbaya ya matukio mabaya yanayosababishwa na usimamizi mbaya wa umati na kulegalega kwa usalama.
Mnamo mwaka wa 2008, mahujaji 224 waliuawa na zaidi ya 400 walijeruhiwa katika mkanyagano kwenye hekalu la mlima katika mji wa Kaskazini wa Jodhpur.