Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Edward Mpogolo, ameagiza kukamilishwa kwa miradi yote ya maendeleo wilayani humo ili iweze kuwanufaisha wananchi ipasavyo. Agizo hilo limetolewa siku ya Jumatano katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, na miundombinu ya barabara.
Akiwa katika kituo cha afya Mvuti kilichopo kata ya Msongola, Mpogolo alipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Jiji la Dar es Salaam, Zaituni Hamza. Kituo hicho, kilichojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 500, kinatarajiwa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi huku kikipunguza msongamano katika hospitali za rufaa mara kitakapoanza kutumika.
Katika sekta ya elimu, Mpogolo alikagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari Kigenzi iliyopo kata ya Buyuni na Yongwe iliyopo kata ya Chanika, ambapo aliagiza shule hizo ziwe tayari kuanza kupokea wanafunzi ifikapo Aprili Mosi mwaka huu. Ujenzi wa shule hizo umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Yongwe, Carl Chiwangu, ameeleza kuwa mradi huo ulipokea shilingi milioni 350 chini ya mpango wa Kishindo cha Mama, fedha zilizotumika kujenga madarasa sita, ofisi mbili, maabara, na jengo la utawala pamoja na miundombinu mingine.
Aidha, Mpogolo amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala, Elihuruma Mabelya, kwa juhudi zake za kuhakikisha miradi yote iliyokwama inakamilika na kuanza kutumika kwa wakati.