Latest Posts

MKUU WA WILAYA ILALA APIGA MARUFUKU KILIMO BONDE LA MAGORE, AONYA ATHARI

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametangaza marufuku ya shughuli zote za kilimo katika Bonde la Magore Kibeberu, kata ya Mzinga, Mkoani Dar es Salaam. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya daraja kuvunjika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya pande mbili za eneo hilo.

Akiwa ziarani katika wilaya hiyo siku ya Jumatano, Mpogolo ameweka wazi kuwa marufuku hiyo inaanza kutekelezwa mara moja, huku mkandarasi akiendelea na juhudi za kurejesha mawasiliano katika hali ya kawaida.

Akizungumza na viongozi wa serikali ya mtaa, wananchi na wakulima wa eneo hilo, amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria za matumizi ya ardhi, hasa kuheshimu umbali wa mita 60 kutoka barabara inapoanzia.

Ameeleza kuwa athari za kilimo holela katika bonde hilo ni pamoja na kutanuka kwa mto, hali inayosababisha kuhama kwa mkondo wa maji kutoka njia yake ya asili na kusababisha maji kupita nje ya makaravati, jambo linalochangia uharibifu wa miundombinu.

Katika hatua nyingine, Mpogolo amemwagiza mkandarasi anayehusika na ujenzi wa daraja hilo kuhakikisha njia za maji zilizoziba zinafunguliwa haraka ili kurejesha mifumo sahihi ya mtiririko wa maji.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mzinga, Isac Job, amepongeza hatua za haraka zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya kuhakikisha mawasiliano yanarejea. Naye Meneja wa TARURA Wilaya ya Ilala, Eng. Magori, amemhakikishia Mpogolo kuwa atasimamia kwa bidii ujenzi wa daraja hilo ili kuhakikisha wananchi na watumiaji wengine wa barabara wanaendelea kupata huduma bila matatizo.

Aidha, madereva wa magari makubwa wametakiwa kuepuka kupitisha magari yenye mizigo mizito isiyoendana na uwezo wa daraja hilo ili kuepusha uharibifu zaidi wa miundombinu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!