18 Septemba, 2024
Bukoba
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mheshimiwa Erasto Sima tarehe 18 Septemba, 2024 amewataka walimu wakuu katika wilaya hiyo kuhakikisha wanaimarisha usimamizi wa Taaluma kwakuwa wao ndio watendaji wakuu wa shule.
Mheshimiwa Sima ameyasema hayo wakati wa ugunguzi wa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa walimu wakuu wa Mkoa wa Kagera ambapo kwa wilaya ya Bukoba yanaendeshwa katika kituo cha shule ya sekondari Kashozi kuanzia tarehe 17-19 Septemba, 2024.
“Walimu wakuu ni wasimamizi wa shughuli zote za uendeshaji shuleni ikiwa ni pamoja na taaluma, miradi ya maendeleo, nidhamu, malezi na shughuli zingine zinazochagiza maendeleo ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni, hivyo hakikisheni mafunzo haya yanaleta tija katika wilaya ya Bukoba kwa kuhakikisha mtakaporudi katika vituo vyenu mnakwenda kuwa wasimamizi imara wa mambo hayo”. Amesema Mheshimiwa Sima
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Bi. Fatina Laay akizungumza na walimu wakuu wanaoshiriki mafunzo hayo amewataka walimu wakuu hao kuhakikisha wanakuwa watulivu na makini kipindi chote cha mafunzo ili yawajengee uwezo wa kutosha hasa katika uendeshaji wa Ofisi ya Mwalimu Mkuu, utunzaji wa takwimu na rasilimali za shule na kusimamia malezi na usalama wa wanafunzi shuleni.