Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bara, Stephen Wasira, amewataka wanachama wa CCM katika wilaya za Karagwe na Kyerwa kupunguza matumizi ya fedha katika michakato ya uchaguzi wa ndani ya chama.
Akizungumza na wanachama wa CCM siku ya Jumapili mkoani Kagera, Wasira amekemea vikali tabia ya baadhi ya wagombea kutumia fedha kuhonga wapiga kura badala ya kutegemea maoni halali ya wanachama.
“Mnazidi mno kufanya chaguzi za pesa, biashara gani hiyo? Mwenyekiti wa CCM Kyerwa, waambie watu wako wapunguze sana hela. Wanapata hela za kahawa, lakini siyo kazi ya hela ya kahawa kuhonga,” amesema.
Wasira, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM amesema ana taarifa za kina kuhusu wagombea wanaotumia fedha kununua uungwaji mkono na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Unajua mimi ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM, kazi yangu ni hiyo kucheki cheki. Sasa Kyela mnagawa hela sana! Ninataka niwaambie kuwa tunachunguza na tunajua, na wale magwiji wa kugawa hela tutawaondoa katika orodha ya wagombea.”
Katika hotuba yake, Wasira ameeleza kuwa chama kimeweka utaratibu wa wagombea kupita kwa mabalozi wa nyumba kumi ili kupata maoni ya wananchi kwa uwazi.
“Tumeweka wagombea waende kwa mabalozi wa nyumba kumi ili kuongeza wigo wa wapiga kura. Mabalozi hawa ni daraja muhimu kwa sababu wanaishi na wananchi, wanajua wananchi wanasemaje.”
Hata hivyo, alilalamikia tabia ya baadhi ya wagombea kuwahonga mabalozi kwa “shilingi elfu kumi kumi”, akisema kuwa hiyo inapotosha mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama.
“Wasa mabalozi acheni kuhongwa. Tunataka watu wanaokubalika na wananchi, si wanaonunua uungwaji mkono kwa hela.”
Wasira ameonya kuwa ikiwa CCM itaendelea na tabia hii ya rushwa katika chaguzi zake, chama kinaweza kujikuta kwenye mgawanyiko mkubwa unaowanufaisha wapinzani.
“Mkileta mtu ambaye hafai, watu wetu watagawanyika. Wakigawanyika, wapinzani wanapita katikati yetu. Badala ya kupiga kura ya furaha, wanachama watapiga kura za hasira, na hilo ni tatizo kubwa.” Ameeleza.
Amewataka wanachama wa CCM kujirekebisha na kutubu dhambi zao ili chama kiweze kuendelea kushinda kwa misingi ya demokrasia halisi badala ya rushwa ya kisiasa.