Oktoba 8, 2024, wawakilishi wa Asasi za Kiraia (Azaki) pamoja na Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) walitembelea Makao Makuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mikocheni, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi zao za kutembelea vyama vya siasa kwa lengo la kukabidhi Ilani ya Uchaguzi ya Asasi za Kiraia kwa kipindi cha 2024 hadi 2029.
Katika ziara hiyo, THRDC ikishirikiana na zaidi ya asasi 300, ilikabidhi vitabu vya Ilani ya Uchaguzi kwa chama hicho cha upinzani. Mratibu Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, alisema kuwa lengo kuu la kutoa Ilani hiyo kwa vyama vyote vya siasa ni kuhakikisha masuala muhimu kwa ustawi wa Watanzania yanapewa uzito, hasa kuelekea chaguzi mbili zijazo, yaani Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Wakili Olengurumwa alieleza kuwa Ilani hiyo inabeba mawazo chanya na mapendekezo yaliyokusanywa kwa lengo la kutoa mwongozo wa uchaguzi wa haki, uhuru wa kujieleza, na haki za binadamu. Alisisitiza kuwa suala la mchakato wa Katiba Mpya limepewa nafasi kubwa, kwani ndilo linalotarajiwa na Watanzania wengi.
“Ilani hii ni mkusanyiko wa mawazo chanya na mapendekezo ambayo yamezingatia masuala muhimu kwa ustawi wa taifa letu, ikiwa ni pamoja na uzingatiwaji wa haki za binadamu, uchaguzi huru na wa haki, na mchakato wa Katiba Mpya ambayo kila Mtanzania anatamani ije mapema,” alisema Wakili Olengurumwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alipokea nyaraka hizo na kupongeza juhudi za Azaki na THRDC kwa kuandaa Ilani hiyo. Mnyika alisema kuwa baada ya kupitia kwa kina Ilani hiyo, aligundua kuwa ipo sambamba na malengo ya chama chake na inaakisi matakwa ya Watanzania wengi. Alisema CHADEMA itaitumia Ilani hiyo kama nyenzo muhimu katika harakati za kuelekea uchaguzi.
“Nimeipitia Ilani hii kwa kina kabla ya kuipokea rasmi, na nithibitishe kuwa ipo vizuri kabisa. Imekidhi matakwa ya wananchi na kwa kweli haina tofauti na malengo ya Ilani ya CHADEMA. Tutaifanyia kazi kwa umakini na kuhakikisha tunayatekeleza yale yanayowagusa Watanzania,” alisema Mnyika.
Azaki na THRDC zipo katika harakati za kutembelea vyama vyote vya siasa nchini kwa lengo la kukabidhi Ilani ya Uchaguzi ya Asasi za Kiraia kwa kipindi cha 2024-2029.