Mfanyabiashara maarufu wa Tanzania, Mohamed Dewji, ametajwa na jarida la Forbes (2025) miongoni mwa matajiri wakubwa duniani, akiwa na utajiri wa dola bilioni 2.2 (sawa na TZS trilioni 5.7). Dewji, maarufu kama Mo, ameshika nafasi ya 12 kati ya matajiri wa Afrika na ndiye tajiri namba moja katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa orodha ya Forbes ya mwaka 2024, utajiri wa Dewji uliongezeka kutoka dola bilioni 1.5 hadi bilioni 1.8, jambo lililomfanya kuwa mfanyabiashara pekee anayetajwa wazi kuwa bilionea katika Afrika Mashariki na Kati.
Mnamo 2024, alishika nafasi ya 12, akilingana na Strive Masiyiwa, mfanyabiashara mzaliwa wa Zimbabwe anayeishi London.
Katika orodha ya hivi karibuni Aliko Dangote kutoka Nigeria ameshika namba moja akiwa na utajiri wa Dola za Kimarekani Shilingi bilioni 23.9, akifuatiwa na Johann Rupert & familia (Afrika Kusini) – $14B, Nicky Oppenheimer & familia (Afrika Kusini) – $10.4B, Nassef Sawiris (Misri) – $9.6B, Mike Adenuga (Nigeria) – $6.8B, Abdulsamad Rabiu (Nigeria) – $5.1B, Naguib Sawiris (Misri) – $5B, Koos Bekker (Afrika Kusini) – $3.4B, Mohamed Mansour (Misri) – $3.4B, Patrice Motsepe (Afrika Kusini) – $3B na Issad Rebrab & familia (Aljeria) – $3B.
Dewji alirithi biashara ya familia, MeTL Group, kutoka kwa baba yake, Gulam Dewji, ambaye naye aliirithi kutoka kwa baba yake. Biashara hiyo ya kizazi cha tatu ilianza miaka ya 1970, babu wa Dewji wakiwa wauzaji wa sukari katika kiwango kidogo.
Chini ya uongozi wa baba yake, MeTL ilikua kutoka biashara ya kawaida ya uagizaji na usafirishaji hadi kufikia thamani ya dola milioni 30 pale Dewji aliporithi kampuni hiyo.
Safari yake ya biashara ilijengwa kwa hatua. Baba yake alimtambulisha kwenye biashara ya kimataifa akiwa mdogo, akimsafirisha kwenda China, Thailand, Misri, na Marekani kwa ziara za kibiashara. Ziara yake ya kwanza ya biashara ilikuwa China akiwa na umri wa miaka 12, akitembelea miji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Hong Kong.
Baada ya kusoma masuala ya fedha na biashara ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Georgetown, Dewji alifanya kazi kwenye biashara ya familia wakati wa likizo. Baada ya kuhitimu, alianza kutoka ngazi ya chini, akihusika katika logistics, ukaguzi wa fedha, uagizaji na usafirishaji wa bidhaa, kabla ya kuwa Mkurugenzi wa Fedha, Mkurugenzi Mtendaji (CEO), na sasa Rais wa MeTL Group.
Leo, MeTL ina zaidi ya 126 ya biashara katika sekta mbalimbali kama chakula na vinywaji, kilimo, viwanda, na nguo, ikiwa na viwanda 40 vya uzalishaji. Dewji anapanga kuingia kwenye sekta za benki, huduma ndogo za kifedha (microfinance), na a teknolojia ya fedha (FinTech), huku akipanua biashara zake Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, na Mashariki ya Kati. Pia anapanga kuwekeza kwenye sekta ya utalii Zanzibar na hifadhi za taifa Tanzania.
Mo Dewji anasisitiza umuhimu wa utawala bora, uadilifu, uvumilivu, na kuchukua tahadhari katika maamuzi ya kibiashara, akiamini kwamba “hakuna lifti ya kukufikisha kwenye mafanikio, lazima upande ngazi”.
Chini ya uongozi wake, MeTL imepanuka na kuwa kampuni ya kimataifa, ikiwa na masoko Afrika Mashariki, Afrika ya Kati, Kusini mwa Afrika, na hata mataifa ya mbali kama India, Thailand, Italia, na Vietnam.
“Kushinda soko la ndani lilikuwa mwanzo tu,” anasema Dewji, akieleza kuwa MeTL inachangia zaidi ya asilimia 3 ya Pato la Taifa (GDP) la Tanzania.
Baada ya jaribio la utekaji nyara mwaka 2018, Dewji aliharakisha upanuzi wa biashara zake kimataifa, akijitengenezea sifa ya kuwa mjasiriamali wa kimataifa anayelenga athari chanya kwa jamii.
“Sijawahi kutegemea Afrika pekee kwa mafanikio yangu. Ingawa Afrika ni nyumbani kwangu, tunafanikiwa pia Asia, Mashariki ya Kati, na Ulaya, ambako ubunifu na athari za biashara zinakutana,” anasema.
Dewji anaamini katika kuwezesha wananchi kwa kuwekeza katika sekta zilizosahaulika, hasa kilimo. Amefufua mashamba ya mkonge na ameanzisha Mo Cola, akilenga kushindana na kampuni kubwa za kimataifa katika sekta ya vinywaji.
MeTL ni mwajiri wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania baada ya serikali, ikiwa na wafanyakazi 40,000 katika biashara zake 126. Malengo yake ni kufikia wafanyakazi 100,000.
“Nimejifunza kwamba kinachojali zaidi siyo pesa unazotengeneza, bali athari unayokuwa nayo kwenye jamii, idadi ya ajira unazozalisha na maisha unayobadilisha,” anasema Dewji.
Mbali na biashara, Dewji ameleta mageuzi makubwa kwenye soka la Tanzania, hasa katika klabu ya Simba SC, ambako ni rais na mwekezaji mkuu.
Chini ya uongozi wake, Simba SC imekuwa moja ya timu saba bora barani Afrika, ikishindana kwenye michuano ya CAF. Ameanzisha mishahara rasmi kwa wachezaji, akibadilisha mfumo wa zamani ambapo baadhi yao walilipwa kiasi kidogo kama TSH 50,000.
“Nataka kuwekeza kwenye klabu ya Ulaya ili kuunganisha mpira wa Afrika Mashariki na ligi kubwa kama English Premier League,” anasema Dewji, shabiki wa Arsenal.
Pia, ameonesha nia ya kuwekeza katika ndondi, akiamini kuwa Tanzania ina vipaji vikubwa katika mchezo huo. “Hii ni njia ya kuwasaidia vijana kutoka kwenye umaskini,” anasema.
Kupitia Mohammed Dewji Foundation (MDF), Dewji ameleta mabadiliko makubwa kwenye upatikanaji wa maji safi Tanzania. Kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, MDF imechimba visima katika maeneo mbalimbali, kufanikisha upatikanaji wa maji kwa zaidi ya watu 11,350. Mpango wa 2024 unalenga kujenga visima vipya 50 na kukarabati vingine 50, kusaidia watu 15,000 zaidi.
Katika sekta ya afya, MDF inatoa huduma za macho, zikiwemo upasuaji wa katarakti na utoaji wa miwani. Pia, inasaidia watoto wenye spina bifida na hydrocephalus, ikifadhili upasuaji na matibabu ya baada ya upasuaji.
Mnamo 2016, Dewji alijiunga na The Giving Pledge, akiahidi kuchangia angalau nusu ya utajiri wake kwa shughuli za kijamii. “Huu ni wajibu wangu, uliotokana na imani na maadili ya familia yangu,” anasema.
Kwa miongo kadhaa, Mo Dewji ameendelea kuwa mwekezaji wa kimataifa, kiongozi wa biashara, na mfadhili wa jamii. Kupitia MeTL na MDF, ameonesha kwamba uongozi wa kifedha na uwajibikaji kwa jamii vinaweza kwenda sambamba.