Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) ambayo ipo chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake Mhandisi Tamimu Katakweba imeibuka mshindi wa nafasi ya 3 kati ya mamlaka za maji 84 nchini katika utoaji wa taarifa na habari kwa wananchi.
Hilo limebainika wakati Msemaji Mkuu wa Serikali Thomas Makoba akisoma taarifa hiyo Jumanne Juni 18, 2024 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini linaloendelea katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam ambalo pia litaambatana na Kikao Kazi cha Maafisa Habari wa Serikali kitakachoanza tarehe 20 Juni, 2024.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye anatarajiwa kukabidhi tuzo kwa mamlaka zilizofanya vizuri kwa niaba ya Rais Samia siku ya kufunga kongamano hilo tarehe 22 Juni, 2024.