Latest Posts

MPINA AGOMEA WITO WA TUME YA RAIS YA KUCHUNGUZA MATUKIO YA OKT. 29

Mwanachama mwandamizi wa chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Joelson Mpina, amekataa rasmi wito wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, akisisitiza kuwa hatatoa ushirikiano wowote kwa chombo hicho.

Katika barua yake ya tarehe 30 Januari 2026, iliyoelekezwa kwa Katibu wa Tume hiyo, Onorius Njole, Mpina amebainisha kuwa hatahudhuria kikao alichopangiwa kufika tarehe 31 Januari 2026 katika Ukumbi wa Manyara, Benki Kuu jijini Dar es Salaam.

Mpina ameeleza kuwa uamuzi wake unatokana na msimamo rasmi wa chama chake cha ACT Wazalendo uliotolewa Novemba 18, 2025, ambao unapinga na kukataa kuundwa kwa tume hiyo. Ameongeza kuwa chama chake kilikwishatangaza mapema kuwa hakitashiriki kwa namna yoyote katika uchunguzi huo kwa kile walichokiita “chombo kisicho huru.”

“Chama cha ACT Wazalendo kiliweka wazi kwamba hakitashiriki kwa namna yoyote ile katika uchunguzi utakaofanywa na Tume hii. Hatutatoa ushahidi wala kutoa ushirikiano wowote kwani tunatambua kuwa ni chombo kisicho huru na kitakachotegemea maagizo ya Serikali”, ameeleza Mpina katika barua hiyo.

Aidha, Mpina amekumbusha msimamo wake alioutoa Desemba 6, 2025, ambapo alidai kuwa tume hiyo imeundwa bila kuzingatia kanuni na taratibu za kimataifa za usuluhishi wa migogoro (Conflict Resolution Strategies and Guidelines). Kwa mujibu wa Mpina, tume hiyo haina sifa za kufanya uchunguzi wa haki na usawa kutokana na mazingira ya uundwaji wake.

Jambo TV imeutafuta upande wa Tume hiyo kutaka kufahamu zaidi kuhusu wito huo, hata hivyo haikupata majibu kutokana na simu ya Katibu Njole kutopokelewa alipopigiwa, na ujumbe wa maandishi kutojibiwa mpaka taarifa hii inachapishwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!