Latest Posts

MREMA: TAFAKARINI WAPI DAMU ITAMWAGIKA ZAIDI- UCHAGUZI AU MAPAMBANO?

Mwanasiasa nguli na mmoja wa waasisi wa kundi la G-55 ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mrema, amewataka Watanzania na viongozi wa kisiasa kuwa na tafakuri ya kina kuhusu namna bora ya kushiriki mchakato wa kidemokrasia bila kusababisha umwagikaji wa damu.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumapili kwa niaba ya wenzake waliokusanyika jijini Dar es Salaam, Mrema ameeleza wasiwasi wake kuhusu baadhi ya hoja zinazojengwa dhidi ya ushiriki wa vijana katika uchaguzi, akidai kuwa hoja hizo zinapotosha na kuhatarisha amani ya taifa.

“Wapo wanaojenga hoja kwamba kushiriki uchaguzi ni kuwapeleka vijana wakamwage damu, kwamba tuna njaa ya damu, wakati huohuo wakihamasishe tukazuie uchaguzi… hivi itamwagika wakati gani zaidi, wakati wa kushiriki uchaguzi au wakati mapambano na Dola, polisi na majeshi yao wakati wa kuzuia uchaguzi?” amehoji Mrema.

Ameongeza kuwa ni vyema viongozi wakatambua wajibu wao wa kulinda uhai wa kila Mtanzania na kutafuta njia salama ya kushiriki katika mchakato wa kisiasa. Amesisitiza kuwa mapambano ya kweli dhidi ya mfumo kandamizi hufanyika kupitia sanduku la kura, si kwa kuvuruga taratibu zilizowekwa kikatiba.

“Kama tunaweza kuepusha tone la damu la Mtanzania kumwagika, viongozi tuna wajibu wa msingi wa kulinda uhai wa watu wetu,” amesisitiza.

Mrema amebainisha kuwa historia haijawahi kuonesha mafanikio ya harakati za kuzuia uchaguzi kwa nguvu, bali mafanikio ya kweli huja kupitia ushiriki wa moja kwa moja katika michakato ya uchaguzi kwa njia ya amani na kuzingatia misingi ya Katiba.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!