Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeanzisha kampeni ya ukusanyaji madeni ya maegesho ya magari katika maeneo mbalimbali ya halmashauri ya jiji la Dar es Salaam huku ikitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wakati wa zoezi hilo ambapo kwa sasa madeni yanafikia jumla ya Shilingi bilioni 7.5.
Agizo hilo linakuja kufuatia Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa kuagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinakusanya madeni mbalimbali ikiwamo hayo ya maegesho.
Akizungumza na wanahabari Jumamosi Juni 22, 2024, Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema wako kwenye mkakati wa zaidi ya wiki mbili kuhakikisha wanakusanya fedha hizo za madeni ya serikali ambazo zinatokana na maegesho ya magari katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
“Kumekuwa na desturi ya kuegesha magari katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ambapo yamekuwa yakitumia mfumo wa kulipa baada, sasa kwa kipindi cha muda mrefu watu wamekuwa hawalipi maegesho hayo na hivyo kusababisha madeni makubwa yanayofikia bilioni 7.5,” Amesema Mpogolo.
Amesema wako kwenye hatua za mwisho kwa kushirikiana na TAMISEMI kuona ni namna gani wanaweza kurejesha fedha hizo na kuwataka wadaiwa kulipa kupitia tovuti na huduma za simu watakazopewa maelekezo.