Na Stephano Mango, Nyasa
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Nyasa, Khalid Khalif, ametoa wito kwa wadau wa uchaguzi kuhakikisha taarifa za uchaguzi zinawafikia wananchi wa Wilaya ya Nyasa ili waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi la kujiandikisha, kugombea, na kupiga kura. Khalif alisisitiza umuhimu wa ushiriki huo katika kupata viongozi bora watakaosimamia maendeleo ya maeneo yao.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa, ambacho kilihudhuriwa na viongozi wa dini, vyama vya siasa, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, na Kamati ya Usalama ya Wilaya, Khalif alieleza kwamba kanuni namba 9 ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, na Mwenyekiti wa Kitongoji wa mwaka 2024 inampa mamlaka ya kutoa maelekezo kwa wadau siku 62 kabla ya uchaguzi.
Khalif alibainisha kuwa uchaguzi huo utafanyika tarehe 27 Novemba 2024, ambapo Vijiji 84 na Vitongoji 421 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa vitashiriki katika uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji, vitongoji, na wajumbe wa Halmashauri za Vijiji, pamoja na wajumbe wa kundi la wanawake.
Kuhusu zoezi la uandikishaji, alieleza kuwa litafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba 2024 kwenye majengo ya umma katika maeneo husika. Pale ambapo hakutakuwa na jengo la umma, uandikishaji utafanyika sehemu mbadala kwa makubaliano kati ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi na viongozi wa vyama vya siasa.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri, aliwasihi wadau kuhakikisha wanatoa hamasa kwa wanajamii ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo. Pia alisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi bora wenye malengo ya kuleta maendeleo, akiwataka wananchi kumchagua kiongozi mwenye shughuli binafsi za maendeleo ili aweze kuongoza jamii kwa ufanisi.
Wadau wa uchaguzi waliokuwepo walionyesha utayari wao wa kushirikiana na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.