Wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini wananufaika na Bandari ya Mtwara kwa kupata ajira kipindi hiki cha msimu wa korosho 2024/2025.
Wakizungumza baadhi ya vibarua wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali bandarini hapo ikiwemo kupakia korosho kwenye makasha (stuffing) na kufanya usafi wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu zao la korosho kupita kwenye bandari hiyo ya Mtwara.
“Rais Samia kuruhusu korosho kupitia bandari hii siyo wakazi wa Mtwara pekee ambao wananufaika bali ni nchi nzima wapo vibarua wengi kutoka nje ya mkoa huu wanatoka Arusha, Mwanza wote tunao hapa kwahiyo hii ni fursa kwa nchi nzima.” Amesema Saidi Kilazi
Monica John ameiomba serikali kuwa, miaka yote korosho ziweze kusafirishwa kupitia bandari hiyo kwani wanawake wanapata fursa ya kujikwamua kiuchumi na kuweza kuendesha maisha yao kwa uhakika ambapo kwa siku mtu mmoja anaweza kupata elfu 30 kima cha chini.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Usafirishaji wa Bandari Tanzania TPA mkoa wa Mtwara Ferdinand Nyathi amesema makasha zaidi ya 3000 tayari yamepokelewa kwenye bandari hiyo kwa ajili ya kupakia na kusafirisha zao la korosho ghafi kwa msimu wa mwaka 2024/2025.
Amesema bandari hiyo imepokea meli saba ambazo zimeshusha makasha matupu takribani 3,700 ambayo yanaweza kuhudumia hadi tani laki 100,000 ndani ya bandari.
“Tuna matarajio ya kupokea meli nyingi zaidi katika kipindi hiki cha siku nne na kuna meli tatu tayari zimeshafika na zinatarajia kuingia bandarini muda wowote lakini bandari inaendelea kupokea meli nyingi zaidi na wateja wanaendelea kuweka oda kwenye mfumo wetu ambao unaonyesha nia yao ya kuja kushusha na kuchukua makasha katika bandari hii ya Mtwara.” Amesema Nyathi
Pia wanatarajia ndani ya siku za hivi karibuni kupita meli tatu ambazo zinatarajiwa kuingia bandarini hapo na kuanza kusafirisha korosho ambazo zimeshafungashwa kwenye makasha kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nchi za nje.
Ameongeza kuwa endapo tani zote laki 500,000 za korosho ghafi zitasafilishwa kupitia bandari ya Mtwara wao wako tayari kwa kuzihudumia kwa ufanisi mkubwa.