Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amesema kuwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imekuwa ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wenye migogoro ya aina mbalimbali ikiwamo migogoro ya ardhi na kuwasaidia wenye kipato kisichowawezesha kumudu gharama za mawakili na kuondokana na vishoka.
Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo wakati akiwasilisha salamu za Wizara ya Katiba na Sheria katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama Juni 12, 2024.
Akizungumza katika kikao hicho Sagini amesema kuwa katika mkoa wa Njombe ambapo alifanikiwa kushiriki na kushuhudia wananchi wakipata huduma za msaada wa kisheria yakiwamo pia maeneo ya magereza, wananchi wengi wenye migogoro iliyopo mahakamani na nje ya mahakama wameweza kupatiwa suluhu kwenye migogoro hiyo.
“Tunamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, wananchi wengi wamenufaika na wizara itakwenda kuandaa orodha ya watoa huduma za msaada wa Kisheria katika kila mkoa. Lengo ni kila mwananchi mwenye changamoto ya masuala ya kisheria aweze kuondokana na ‘vishoka’ hata baada ya kumalizika kwa kampeni na kumwezesha mwananchi kupata huduma hiyo bila malipo.” Amesema Sagini.
Rai imetolewa kwa wananchi wenye migogoro mbalimbali kwenye maeneo yao hususani changamoto za masuala ya ardhi, wosia na mirathi, ndoa, matunzo kwa watoto na migogoro mingineyo inayohitaji msaada wa kisheria kuhakikisha wanatumia kampeni hii na kuwatumia Watoa huduma za Msaada wa Kisheria ili kupata ushauri kwenye masuala yanayowatatiza badala ya kukimbilia vishoka.