Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuahirisha kwa muda usikilizwaji wa kesi ya kusambaza taarifa za uongo (uchochezi) kupitia mtandao wa YouTube inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kutokana na changamoto za mtandao.
Kesi hiyo, ambayo ilipangwa kuendelea leo Aprili 24, 2025 kwa njia ya video conference mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Geoffrey Mhini, iliahirishwa kwa muda wa dakika 10 baada ya sauti kutokusikika vizuri kupitia mfumo wa mtandao uliotumika.
Kulingana na tovuti ya Mwananchi, Hakimu Mhini amesema kuwa kutokana na hitilafu hiyo, mahakama inaahirisha shauri hilo kwa muda mfupi, na iwapo changamoto hiyo itaendelea, atatoa uamuzi mwingine kuhusu mwenendo wa kesi hiyo.
Kesi hiyo ya kusambaza taarifa za uongo ni miongoni mwa mashauri kadhaa yanayomkabili Lissu, ambaye hajafikishwa mahakamani leo na hivyo kesi zake zinatarajiwa kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Wakati kesi hiyo ikiitwa kwa usikilizwaji wa hoja za awali, ukumbi wa video conference wa mahakama hiyo ulijaa, hali iliyosababisha baadhi ya watu kuzuiwa kuingia kushuhudia mwenendo wa kesi.