Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao imetangaza kushiriki moja kwa moja katika maandalizi ya Mtoko wa Pasaka utakaofanyika Aprili 20 katika ukumbi wa Super Dome, Masaki mkoani Dar es Salaam, ikilenga kuunganisha Watanzania kupitia nyimbo, maombi, na kutoa misaada kwa kina mama wajawazito.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, msanii na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Steven Mengele maarufu kama Steve Nyerere, amesema kuwa tukio hilo litakuwa maalum kwa ajili ya kuliombea taifa na kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan katika mwaka huu wa uchaguzi.
“Amani tuliyopewa na Mungu lazima tuilinde kwa gharama yoyote. Maombi yana nguvu kuliko mtutu wa bunduki,” amesema Nyerere kwa msisitizo.
Taasisi hiyo pia imetangaza kutoa msaada kwa kina mama wajawazito katika hospitali zote za wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam kuelekea kilele cha Pasaka.
“Akina mama sasa hivi ndio wanaobeba taifa. Hii fursa ya kuwasaidia ni sehemu ya kazi yetu kama taasisi yenye lengo la kuongelea na kugusa maisha ya Watanzania kwa vitendo,” ameongeza.
Miongoni mwa matukio makuu kwenye Mtoko wa Pasaka ni maonesho ya muziki wa Injili, ambapo mwanamuziki nyota Christina Shusho, ambaye pia ni mwanachama wa Mama Ongea na Mwanao, atatumbuiza pamoja na wasanii wengine wa Injili kutoka ndani na nje ya Tanzania.
“Mtoko huu utakuwa wa kipekee. Ni mwaka wangu wa tatu tangu kuanzishwa kwake. Lengo kuu ni kuwaleta Watanzania na Afrika Mashariki pamoja katika amani na mshikamano,” amesema Christina Shusho, akielezea pia dhamira ya kuwaombea viongozi, hususan Rais Samia.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kwa Maombi Utashinda”, ikiwa ni ujumbe mahsusi kwa Watanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi, huku wasanii wa Injili wakionesha mshikamano wao na kuonesha kuwa “wanamtakia mema Rais wao.”