Na Amani Hamisi Mjege.
Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umesimamisha shughuli za kivuko cha MV. Kigamboni kwa watumiaji wa kivuko Magogoni Kigamboni na wananchi kwa ujumla kuanzia siku ya Ijumaa tarehe 07 Juni, 2024.
Taarifa iliyotolewa na TEMESA siku ya Alhamisi imeeleza kuwa kivuko hicho kinasimama kutoa huduma ili kufanyiwa ukarabati mkubwa kabla ya kurejea kutoa huduma kikiwa katika hali ya ubora na usalama.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa shughuli za uvushaji katika eneo hilo zitaendelea kutolewa kama kawaida kwa kutumia kivuko Mv. Kazi pamoja na Sea Taxi, boti iliyodiwa kutoka kampuni ya Bakhresa.
TEMESA imewashauri abiria hasa wenye magari kutumia njia mbadala ya Daraja la Mwalimu Nyerere ili kuepusha msongamano katika eneo la kivuko mpaka pale kivuko hicho kitakaporejea.Â
Hata hivyo taarifa ya kituo cha habari cha Mwananchi ya siku ya Ijumaa inaeleza kuwa bado katika eneo hilo kumeshuhudiwa magari yakivushwa na kwamba ni kivuko cha Mv Kazi pekee ndicho kilichoonekana kikivusha abiria saa 1:07 asubuhi, huku kivuko kimoja cha Sea Tax kikishuhudiwa kikiwa kimeegeshwa upande wa Magogoni (Posta) sambamba na kivuko cha Mv. Kigamboni kinachotarajiwa kufanyiwa ukarabati.
Hii si mara ya kwanza kwa kivuko hiki kupelekwa kwenye matengenezo makubwa, kwani mwaka 2014 kivuko cha Mv. kigamboni kilipitia hali hiyo na huduma za uvushaji watu pamoja na magari zikatolewa na vivuko vya Mv. Magogoni pamoja na Mv. Lami katika kipindi chote cha matengenezo.
Taarifa ya TEMESA ya hivi karibuni inakuja wakati ambao kuna ukarabati mwingine mkubwa wa kivuko cha Mv. Magogoni unaoendelea Mombasa nchini Kenya ambao unaelezwa kufikia hatua nzuri ukitarajiwa kukamilika Disemba 2024 kwa mujibu wa kauli ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya aliyoisema Alhamisi Mei 30, 2024 katika kikao cha Bunge jijini Dodoma wakati akijibu hoja za Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile.
Kulingana na taarifa iliyochapishwa na tovuti ya TEMESA, Februari 16, 2023, ukarabati wa kivuko cha Mv. Magogoni unagharimu shilingi Bilioni 7.5 huku ukifanywa na African Marine and General Engineering Company Ltd. Bado gharama za ukarabati wa Mv. Kigamboni haujawekwa wazi.