Latest Posts

MVUA YATAJWA KUCHELEWESHA UJENZI WA BARABARA TARIME NA SERENGETI

‎‎Na Helena Magabe-Musoma

 

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mara, Mhandisi William Lameck, amesema mvua zinazoendelea kunyesha kwa muda mrefu katika wilaya za Tarime na Serengeti zimekuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara.

Akizungumza na Jambo TV ofisini kwake, Mhandisi Lameck alifafanua kuwa baadhi ya barabara tayari zilishatengewa fedha kwa ajili ya kutengenezwa, lakini mvua zimekuwa zikiingilia kati utekelezaji wa kazi hizo, hasa kutokana na kukosekana kwa hali ya hewa rafiki kwa ujenzi na ugumu wa mazingira ya barabara na mito kujaa maji.

“Mvua ni changamoto kubwa sana hasa Tarime na Serengeti. Unakuta barabara imetengewa bajeti lakini mvua inaanza, mkandarasi anashindwa kuanza kazi, magari hayawezi kubeba kifusi na hata mito imejaa huwezi hata kutengeneza daraja,” alisema Lameck.

Bajeti Kidogo Kwenye Mahitaji Makubwa

Mhandisi Lameck alitaja uhaba wa bajeti kuwa changamoto ya kitaifa, akieleza kuwa ingawa TARURA inaweza kuwasilisha ombi la bajeti ya shilingi bilioni 10, mara nyingi hupatiwa kiasi kidogo kama bilioni 1 tu.

“Mahitaji ya barabara ni makubwa sana nchi nzima, lakini fedha ni chache. Tunapewa asilimia 10 tu ya kile tunachoomba. Tunabana matumizi ili angalau kutengeneza barabara zenye changamoto kubwa zaidi,” aliongeza.

Barabara Zaidi Zipo Kwenye Mpango wa Ujenzi Tarime Mjini

Alizitaja baadhi ya barabara zilizo kwenye mpango wa kutengenezwa katika Jimbo la Tarime Mjini kuwa ni pamoja na:

  • Barabara ya Nyerere
  • NMB Market
  • Market RC
  • Mennonite
  • Mara Coffee
  • Market Ronsonti
  • Saronge “A”
  • Amazon
  • Boma One hadi Boma Four

Lengo kuu, alisema, ni kupunguza idadi ya barabara za vumbi na kuzibadilisha kuwa za changarawe kadri fedha zitakavyopatikana, ili ziweze kudumu mwaka mzima hata wakati wa mvua.

Taa za Barabarani na Mipango ya Baadaye

Kuhusu kuwekwa kwa taa katika barabara za vumbi, Mhandisi Lameck alisema:

“Ni kweli barabara zote zinastahili kuwa na taa, lakini barabara za vumbi zikipewa taa kabla ya kuwekwa lami, gharama huongezeka tena ikifika wakati wa kuweka rami. Hivyo ni vyema taa zikawekwa baada ya hatua hiyo.”

Ameongeza kuwa wabunge au halmashauri wanaweza kusaidia kuweka taa hasa kwenye maeneo ya biashara.

Mchakato wa Zabuni kwa Wakandarasi

Kwa mujibu wa Mhandisi Lameck, zabuni za kazi za TARURA hutangazwa kupitia mfumo wa kitaifa wa manunuzi wa PPRA unaoitwa NeST. Mkandarasi yeyote nchini anaweza kushiriki ikiwa anakidhi vigezo vya usajili vilivyowekwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB).

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!