Latest Posts

MWABUKUSI: MFUMO WA SIASA NCHINI UNAHITAJI MAGEUZI

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amesema kuna haja ya mamlaka kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa na wagombea binafsi ili kukuza ushindani wa kisiasa na kuimarisha demokrasia nchini.

‎Akizungumza Septemba 15, 2025, kupitia Clouds TV, Mwabukusi amesema mfumo wa sasa wa uchaguzi una changamoto nyingi, jambo linalodhihirishwa na kaulimbiu za baadhi ya vyama vya siasa ambazo zimebeba malalamiko ya wazi kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi.

‎“Kwa sasa huu mfumo mzima wa demokrasia tumejikwaa. Lakini sasa tufanyeje tusianguke? Hilo ndilo jukumu la TLS tunalolifanya,” amesema Mwabukusi.

‎Alipohojiwa kuhusu hali ya kisiasa nchini, Mwabukusi amesisitiza kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inapaswa kutambua kuwa uchaguzi ni suala la wananchi huku akionya kuwa endapo kutatokea vurugu au uharibifu wowote katika kipindi cha uchaguzi, tume hiyo itapaswa kuwajibika.

‎Kuhusu kuenguliwa kwa mgombea wa nafasi ya Urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Mwabukusi amesema mapingamizi yaliyowekwa dhidi ya mgombea huyo hayaendani na madai ya kukosekana kwa sifa, bali yanaashiria mkakati wa kuvuruga demokrasia.

‎Katika juhudi za kuhakikisha TLS inatoa mchango katika kujenga utulivu wa kisiasa, ameeleza kuwa chama hicho kiliandaa mkutano wa pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na taasisi mbalimbali ili kujadiliana kuhusu mwenendo wa siasa, ingawa baadhi ya vyama havikushiriki.

‎Aidha, Mwabukusi amesisitiza umuhimu wa kuwa na katiba mpya ya wananchi na kufanya mabadiliko ya msingi katika baadhi ya vyombo vya dola, hasa jeshi la polisi. Ametoa wito kwamba jeshi hilo libadilishwe kutoka kuwa “jeshi” hadi kuwa “huduma ya polisi” ili kuendana na mahitaji ya kidemokrasia.

‎Akihitimisha mahojiano hayo, Rais wa TLS amewataka Watanzania kuenzi umoja na kutambua kuwa taifa ni muhimu zaidi kuliko vyama vya siasa, huku akihimiza mshikamano kwa maendeleo ya Taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!