Shirika la Tanzania Aid Association (TAA) kwa udhamini wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) limepanda miti 500 shule ya msingi Mbwanjiki wilayani Ikungi mkoani Singida ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya upandaji miti ya ‘Singida Mpya ya Kijani Inawezekana’ yenye lengo la kuvutia wapenda mazingira nchini kushiriki katika upandaji wa miti.
Â
Mgeni rasmi katika zoezi hilo la upandaji wa miti alikuwa ni raia wa kawaida Jonas Changas aliyepata nafasi hiyo baada ya kumpigia simu Mkurugenzi Mtendaji wa TAA, Suphian Juma Nkuwi kuomba kupanda miti katika shule ya Kijiji anakoishi.
Â
Mkurugenzi Mtendaji wa TAA, Suphian amesema uamuzi wa kumteua raia wa kawaida kuwa mgeni rasmi ni kutokana na nia yake ya dhati ya kutunza mazingira ambayo amekuwa akiionesha kwa kumpigia Nkuwi mara kwa mara.
Â
“Najua si jambo lililozoeleka raia wa kawaida kuwa mgeni rasmi tumezoea viongozi kuwa wageni rasmi, tumemteua bwana Changas kuwa mgeni rasmi baada ya kuonesha mahaba mazito ya kutunza mazingira kwa kunipigia simu mara kwa mara tulete miti shuleni hapa. Hii iwe chachu kwenu wananchi kupenda na kuhifadhi mazingira kuunusuru mkoa na nchi yetu dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi” Ameeleza Nkuwi.
Â
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Singida, Thomas Mgonto amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TAA kwa kuanzisha kampeni ya kihistoria, na kusisitiza kwa wanafunzi na wananchi umuhimu wa kutunza miti ambapo amesema bila miti hakuna maji, na bila maji hakuna uhai, hivyo wananchi waache matumizi mabaya ya miti bila kuirejesha.
Â
Naye Katibu wa Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu kwa niaba yake amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa TAA na TFS kwa kupanda miti jimboni kwake na kutoa salamu za mbunge kama mwakilishi wa wananchi ambapo ameishukuru TAA kwa mwaliko na kwamba anaunga mkono kampeni hiyo akiwataka wananchi kutunza mazingira.
Â
“Ndugu yangu na rafiki wa Mazingira nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa TAA Mheshimiwa Suphian, Mheshimiwa Mbunge Mtaturu anawashukuru TAA kwa mwaliko huu, Mazingira ni afya yetu, miti hututunza, nasi tuitunze iendelee kututunza” Ameeleza Katibu wa Mbunge Mtaturu.
Â
Mgeni Rasmi wa zoezi hilo Jonas Changas amehitimisha mazungumzo kwa kuwataka wanafunzi na wananchi kuitunza miti hiyo kwa udi na uvumba ili kudhibiti ukame ambao ni janga la miongo mingi mkoani Singida.
Â
“Mimi ninaishi hapa kijijini miaka zaidi ya 50, kulikuwa na miti na mapori mazuri, tumeikata tumekaribisha ukame, mvua zimekuwa za kusuasua, tunawaahidi TAA tutaisimamia miti hii, na kipekee mimi mwenyewe kila wiki nitakuwa nakuja hapa kuangalia maendeleo yake, haitowezekana niwekwe kwenye bango kama mgeni rasmi halafu miti ife nipo hapa” Ameeleza Changas.
Mpango wa Shirika la TAA kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa TAA Suphian Juma Nkuwi ni kupanda miti milioni moja mkoa wa Singida katika awamu ya awali lengo likiwa si tu kurejesha uoto uliopotea bali pia kutoa darasa kwa wananchi wote katika kutunza mazingira.